VIBANDA 13 VYA MADUKA KIGOMA VYATEKETEA KWA MOTO

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

VYUMBA 13 vya maduka katika soko la Mwandiga Halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma vimeteketea kwa moto na mali zilizokuwepo kwenye vibanda hivyo zimeungua kabisa.

Kamanda wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma,Augustin Magere alisema hayo akitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alitembelea eneo hilo kuona athari zilizotokeana na kuwapa pole waathirika wa vibanda hivyo.

Kamada huyo wa kikosi cha zimamoto na uokoaji alisema kuwa walipata taarifa ya kutokea kwa moto huo majira ya saa 8:15 usiku wa kuamkia Oktoba 28 na walifika eneo la tukio dakika 15 baadaye na kuweza kuudhibiti moto huo uzilete madhara na kwamba uchunguzi wa tukio hilo umenza akieleza kuwa sehemu kubwa ya vibanda vilivyoathirika ni vya tiba asilia.

 

Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro aliwapa pole wote waliopata na janga hilo na kubainisha kuwa vikosi cha zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na polisi na vyombo vingine wameanza uchunguzi kujua chanzo cha moto huo.

Sambamba na hilo Balozi Sirro alisema kuwa serikali inaendelea kufanya tathmini na kufanya tafakuru hatua za kuchukua kuhusiana na tukio hilo huku akieleza kuwa uchunguzi inafanyika na ikibainika kuna mtu au watu walihusika na moto huo hatua za kisheria zitachukuliwa.

Mwisho.