DAR ES SALAAM: Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuweka mikakati inayotekelezeka ya kuimarisha viwanda, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha rasilimali za ukanda huo zinawanufaisha wananchi kupitia ajira na ukuaji wa biashara.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo na mchumi mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye mkutano wa majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kuhusu minyororo ya thamani ya ngozi, nguo na mafuta ulioandaliwa na Baraza la Afrika Mashariki (EABC) kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika(AFDB) .
Amesema mafanikio ya majadiliano kuhusu maendeleo ya viwanda yanapaswa kupimwa kwa hatua zitakazochukuliwa baada ya mikutano, ikiwemo kuongeza uzalishaji viwandani, kupanua masoko ya wakulima na kuhakikisha wazalishaji wanapata malighafi bora kwa wakati.
“Takwimu zinaonesha umuhimu wa kuweka mazingira bora ya biashara yatakayowezesha viwanda kuongeza uzalishaji, kuwekeza katika teknolojia na kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa,”amesema.
Mshauri wa Biashara na Sera wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Adrian Njau amesema utafiti uliofanywa na taasisi hiyo unaonesha kuwa ukanda huo unaendelea kuagiza bidhaa nyingi zilizokamilika licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha baadhi ya malighafi zinazotumika kuzitengeneza.
Amesema katika sekta ya ngozi, EAC iliuza nje ngozi ghafi na iliyochakatwa kwa sehemu yenye thamani ya takribani dola milioni 46 mwaka 2025, huku ikiagiza viatu, vipuri na bidhaa za ngozi zenye thamani ya takribani dola milioni 566.

Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha uchakataji wa ngozi hadi hatua za mwisho za utengenezaji wa viatu, mikoba na bidhaa nyingine ili kuongeza thamani inayobaki ndani ya ukanda huo.
Njau amesema changamoto zinazokabili viwanda ni pamoja na uhaba wa malighafi za kutosha, mitaji, teknolojia na ujuzi, huku viwanda vingi vikitumia sehemu ndogo ya uwezo wake wa uzalishaji.
Amezitaka nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuoanisha sera za ushuru, kanuni za asili ya bidhaa na mifumo ya ununuzi wa umma ili bidhaa zinazotengenezwa ndani ya EAC ziweze kupata masoko katika nchi zote wanachama.
Ameeleza kuwa mahitaji ya sare za shule, viatu, mashuka ya hospitali na bidhaa nyingine za taasisi za umma yanaweza kuwa soko la uhakika kwa wazalishaji wa kikanda iwapo nchi wanachama zitaweka mifumo inayowapa nafasi bidhaa zinazotengenezwa ndani ya ukanda huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Frank Dafa, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza viwanda vya ndani, lakini bado kuna pengo kati ya uzalishaji wa malighafi na uwezo wa kuzichakata kuwa bidhaa zilizokamilika.
Dafa amesema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kufikia tani 720,000 kwa mwaka, huku uzalishaji wa ndani ukiwa takribani tani 302,000, hali inayosababisha upungufu wa zaidi ya tani 400,000 kwa mwaka.
CTI imependekeza kuimarisha uhusiano kati ya wakulima, wafugaji na viwanda, kuboresha teknolojia, ujuzi na miundombinu, pamoja na kuweka sera zinazochochea uzalishaji wa ndani na matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini.
Silvester Kazi, mjumbe wa kamati ya mradi huo amesema kwa sasa nchi za Afrika Mashariki zinapoteza fursa za kiuchumi kwa kuuza mazao hayo katika hali ghafi na baadaye kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani, zikiwemo nguo, viatu na mafuta ya kula, hali inayochangia fedha nyingi kwenda nje ya ukanda huo.
“Tunataka kuongeza thamani katika mnyororo wa bidhaa hizi, kuanzia nguo, ngozi pamoja na mafuta ya kula, ili ongezeko hilo la thamani lifanyike hapa hapa nchini na siyo nje,” amesema Kazi.
