Matukio Daima Media, Morogoro
Mshikamano uliooneshwa na Watanzania baada ya kufahamu hali ngumu ya kiafya ya Hassan Bryton, mkazi wa Mkata wilayani Kilosa mkoani Morogoro, umeendelea kuwa sehemu ya historia yake baada ya kufariki dunia kabla ya kupata matibabu aliyokuwa akiyahitaji.
Hassan mwenye umri wa miaka 56 amefariki dunia Oktoba 16, majira ya saa 10 jioni, baada ya kukaa zaidi ya miezi minne bila kula kutokana na uvimbe kwenye koo, hali iliyomfanya kutegemea dripu na kushindwa kuendelea na shughuli zake za kuchoma na kuuza mkaa.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Matukio Daima, Watanzania walipata nafasi ya kufahamu changamoto alizokuwa akipitia na hitaji lake la kupata msaada wa fedha ili kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako alikuwa ameandikiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Dada wa Marehemu Bi Amina Mohamed Malenda aliyekuwa akimuuguza Hassan Byton nyumbani kwake, Mtaa wa Mgaza, kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro anasema tarifa hiyo ilichochea mwitikio wa wananchi walioanza kuchangia kwa uwezo wao.
Hata hivyo akasema kifo chake klichotokea nyumbani hapo kimeifanya familia kuelekeza michango iliyopatikana katika mahitaji ya mazishi, badala ya safari ya matibabu iliyokuwa imekusudiwa.
Balozi katika Mtaa aliokuwa akiishi Hassan enzi za uhai wake, Ephraim Kaunya amewashukuru Watanzania walioungana na Wana Mtaa wa Mgaza kuchangia matibabu ya Hassan aliyekuwa akikabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Akasema mazishi ya Hassan yamefanyika Oktoba 16 mwaka huu majira ya jioni katika makaburi yaliyopo Mtaa wa Mgaza, Kata Mindu, Manispaa ya Morogoro.
Naye mkazi mwingine wa mtaa huo, Juliana Thomas, amesema Nia ya Watanzania ilikuwa njema na wameshuhudia mwamko wa watu katika kuitia moyo familia hiyo iliyokuwa na uhitaji na kuwasihi Watanzania kuendelea kushikamana hasa kwa watu wenye uhitaji bila kuchoka.
“Tunatoa shukrani kwa vyombo vya habari kutupa nafasi ya kuwasilisha changamoto ya Hassan, kusaidia kueneza taarifa zake, na kwa kila Mtanzania aliyejitokeza kwa moyo wa kujali, tunatoa pia pole kwa familia, ndugu na wote walioguswa na msiba huu”Amesema Juliana.
Mwisho



