MOROGORO YAANGAZIA FURSA ZA KUONGEZA THAMANI YA MCHELE

 

Matukio Daima Media, Morogoro

WAKULIMA na wadau wa mnyororo wa thamani wa mpunga wametakiwa kuangalia fursa za kuongeza thamani ya zao hilo kupitia utafiti, uchakataji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, badala ya kutegemea zaidi mchele kama chakula cha kawaida.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amesema hayo wakati wa Warsha ya Kuthibitisha na Kusaini Makubaliano ya Pamoja ya Maendeleo ya Sekta ya Mchele kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Dk Mussa akasema mkoa huo una uwezo mkubwa katika uzalishaji wa mpunga ambapo kwa mwaka wanazalisha hadi tani milioni 1.2 huku nchi ikikadiriwa kuzalisha tani milioni nane.

Akasema hatua hiyo inaonesha muhimu wa wataalamu kuchunguza uwezekano wa kutengeneza bidhaa nyingine  zikama sabuni na mvinyo kwa kutumia mchele kama malighafi.

Amesema utafiti wa kutosha unaweza kusaidia kubaini bidhaa zinazoweza kuzalishwa kibiashara, kuongeza thamani ya zao hilo na kutoa fursa za uwekezaji na ajira.

Aidha akawaomba wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga kusaidia uwezekano wa Mkoa wa Morogoro kuwa na  maghala ya kutosha ya kuhifadhi mpunga, kwani maghala yaliyopo ni madogo madogo na hayatoshelezi.

Katika eneo la ubora wa bidhaa, mwakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), John Kapufi, amesema mamlaka hiyo inapanga kuimarisha usimamizi wa aina za mchele kulingana na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kapufi amesema sifa kama harufu, ukubwa wa punje na ubora zinapaswa kuzingatiwa ili bidhaa zitokane na viwango vinavyotambulika sokoni. Aliongeza kuwa usimamizi wa ubora utaenda sambamba na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji, uhifadhi na uchakataji wa mazao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mchele Tanzania, Geoffrey Rwiza, amesema gharama kubwa za uzalishaji na biashara zinahitaji hatua za pamoja, zikiwemo kuboresha upatikanaji wa mikopo, mbegu bora, pembejeo na zana za kilimo.

Amesema wakulima pia wanahitaji kuacha kuchanganya aina tofauti za mchele kwenye gunia moja kwa kuwa hali hiyo inadhoofisha utambulisho wa bidhaa na kuathiri thamani yake sokoni.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani wa Wizara ya Kilimo, Upendo Mdeme, amesema kuongeza tija ni muhimu katika kupunguza gharama za uzalishaji, huku mpunga ukiendelea kuwa zao muhimu kwa usalama wa chakula na upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje.

Aidha Mkuu wa Korido ya Ukanda wa Ukuaji wa Kilimo Tanzania, AGCOT, John Banga, amesema makubaliano ya hiari ya wadau yanaweka msingi wa kuwajibika kwa pamoja katika kutatua changamoto za zao moja. 

Banga amesema kila mdau anapaswa kuwa na jukumu linaloeleweka na muda wa kutekeleza maazimio yaliyokubaliwa.

Afisa Programu wa Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira Asilia (IUCN), Samwel Kajiba, amesema ushirikiano na AGCOT tangu mwaka 2014 umelenga kuongeza tija katika kilimo huku ukihifadhi mazingira.

 Amesema kupitia mradi wa Sustain katika maeneo ya Morogoro na Iringa unahimiza mifumo endelevu ya uzalishaji, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika na uhifadhi wa bioanuwai.

Wadau hao wameeleza kuwa kuimarisha sekta ya mchele kunahitaji kuunganisha uzalishaji na uhifadhi wa mazingira, mikopo, ubora, uchakataji na masoko ili kuongeza mapato na ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Warsha hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Agricultural Growth Corridors of Tanzania (AGCOT), yaani Ukanda wa Ukuaji wa Kilimo Tanzania, na International Union for Conservation of Nature (IUCN), Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira Asilia ukikutanisha washiriki kutoka Mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya.