Mfanyabiashara Bunju Afikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma Za Kumuua Mkewe

Global Publishers
October 15, 2026
18 views
0 Comments

DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara na mkazi wa Bunju A, jijini Dar es Salaam, Laurence Kweka (48), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na tuhuma za kumuua mkewe, Jane Maloo Urassa, kwa kumpiga risasi.

Kweka amesomewa shtaka hilo leo Alhamisi, Oktoba 15, 2026, na Wakili wa Serikali, Harrison Lukosi, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kemilembe Josiah, katika kesi ya mauaji namba 23407 ya mwaka 2026.

Akisoma shtaka hilo, Wakili Lukosi amedai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 1, 2026, katika eneo la Bunju A, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo anadaiwa kumuua Jane Maloo Urassa kwa kumpiga risasi.

Tuhuma hizo zinadaiwa kuwa kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kabla ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Josiah alimweleza mshtakiwa kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Aidha, hakimu alimweleza Kweka kuwa shtaka la mauaji analokabiliwa nalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ataendelea kusalia rumande hadi upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika.

Kesi hiyo inahusu tuhuma za mauaji zinazodaiwa kutokea katika makazi ya wanandoa hao eneo la Bunju A, jijini Dar es Salaam, huku hatua zinazofuata za kisheria zikisubiri kukamilika kwa upelelezi.

Nifupishie habari hii kwa mtindo wa vyombo vya habari