Meneja Mkuu Mwandamizi wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, ametoa wito kwa serikali za Afrika, wawekezaji na kampuni za teknolojia kujenga mazingira rafiki ya ubunifu yatakayowezesha ukuaji wa teknolojia kuchochea biashara zenye tija, huduma salama na fursa mbalimbali za kujipatia kipato.
Akizungumza katika mkutano wa Sahara Sparks 2026 mbele ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, baadhi ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wageni mbalimbali, Kanyankole alieleza dhamira ya Bolt kutumia teknolojia ya usafiri kuongeza fursa za kipato kwa vijana barani Afrika, ikiwemo Zanzibar.
Katika mjadala wenye kaulimbiu “Navigating the Age of Abundance,” alisema teknolojia inabadilisha sekta ya usafiri Afrika Mashariki kutoka mfumo uliogawanyika na unaotegemea zaidi umiliki wa vyombo vya usafiri, kwenda katika soko rasmi la kidijitali linalofanya kazi kwa wakati halisi.
“Leo wateja wanatarajia gharama nafuu, madereva waliothibitishwa, uwezo wa kufuatilia safari na msaada wa haraka wa kiusalama. Wakati huohuo, madereva wanaweza kuchagua lini, wapi na kwa muda gani wafanye kazi, huku Serikali ikiwa na nafasi ya kusimamia sekta na kuhakikisha usalama unazingatiwa.
Teknolojia hivyo inarahisisha usafiri, inaongeza usalama, inazalisha kipato kwa madereva na kuwawezesha wananchi kuokoa gharama. Katika maeneo kama Moshi, Arusha na Iringa, watalii wanaweza kusafiri kwa ufanisi zaidi na kwa gharama nafuu, hivyo kutumia fedha wanaazookoa katika shughuli nyingine za uchumi wa maeneo hayo, ikiwemo ununuzi,” alisema.
Kanyankole alisema usafiri unapaswa kutazamwa kama sehemu muhimu ya miundombinu ya uchumi.
Takwimu za Bunge zinaonesha sekta ya usafirishaji ilikua kwa asilimia 4.1 na kuchangia takribani asilimia 7.2 ya Pato la Taifa mwaka 2023. Kati ya Julai 2024 na Machi 2025, sekta hiyo iliingiza takribani dola bilioni 2.48 za Marekani katika mapato ya fedha za kigeni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Wizara ya Fedha pia ilihusisha sehemu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania wa asilimia 5.5 mwaka 2024 na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya usafiri pamoja na kuanza kwa huduma za abiria za Reli ya Kisasa (SGR).
Katika usafiri wa kidijitali, maelfu ya madereva nchini Tanzania wanajipatia kipato kupitia Bolt, huku madereva wanaofanya vizuri zaidi wakifikisha hadi Sh3.5 milioni kwa mwezi, hali inayoonesha namna teknolojia ya Bolt inavyobadili mahitaji ya usafiri kuwa chanzo cha riziki kwa wananchi.
Kanyankole alisema hatua zaidi zinahitaji sera na kanuni zinazotabirika, upatikanaji wa mitaji kwa gharama nafuu, ujuzi wa teknolojia nchini na ushirikiano mpana kati ya Serikali na sekta binafsi. Wakati Tanzania ikielekea katika azma ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja, huduma za usafiri wa mtandao tayari zinachangia kurasimisha shughuli za wajasiriamali, wakiwemo madereva wanaowezesha miji kusonga kila siku.





