Meli Yawaka Moto Watu 3 Wafariki, 40+ Waokolewa Ziwa Nyasa

Global Publishers
October 11, 2026
30 views
0 Comments

Watu watatu, wakiwamo raia wa Msumbiji, Malawi na Tanzania, wamefariki dunia baada ya meli ya MV Chambo kushika moto katika Ziwa Nyasa, mkoani Ruvuma, leo Jumapili, Oktoba 11, 2026.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa 10:30 alfajiri, wakati meli hiyo iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Tanzania na Msumbiji ikielekea nchini Msumbiji ikiwa na abiria 44 pamoja na tani 10 za mizigo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peresi Magiri, amesema abiria waliokuwamo kwenye meli hiyo walikuwa raia wa mataifa mbalimbali, wakiwamo raia wanne wa Malawi, 23 wa Msumbiji, 15 wa Tanzania na wawili wa Lesotho.

Amesema watu watatu wamepoteza maisha katika ajali hiyo, wakiwamo mtoto wa kike raia wa Msumbiji, mwanamke raia wa Malawi na Mtanzania aliyetambuliwa kwa jina la Yuston Chatanda, mkazi wa Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, zaidi ya watu 40 wameokolewa kufuatia ajali hiyo, huku juhudi za kufahamu kwa kina mazingira ya tukio hilo zikiendelea.

Hadi sasa, chanzo cha moto uliosababisha meli hiyo kushika moto hakijaelezwa katika taarifa iliyotolewa.

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu mazingira ya usalama wa usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa, ambalo ni njia muhimu ya usafiri na biashara inayounganisha Tanzania na Msumbiji.