Na Matukio Daima Media
Mfanyabiashara na kada wa chama cha Mapinduzi (CCM)Fred Ngajilo maarufu kwa jina la Vunjabei ametoa salamu za majonzi kufuatia kifo cha aliyekuwa Katibu mstaafu wa CCM Mkoa wa Iringa, Said Goha, akieleza kuwa walikutana siku moja kabla ya ajali iliyosababisha kifo chake.
Katika salamu zake za rambirambi, Vunjabei amesema siku moja kabla ya ajali hiyo, Goha alifika ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam, ambako walipata nafasi ya kutazama pamoja mchezo wa soka kati ya Simba na Yanga wakiwa na watumishi wa kampuni ya Vunjabei.
Amesema baada ya kumalizika kwa mchezo huo, waliwasiliana kwa njia ya simu na watu mbalimbali, akiwemo mke wa marehemu, Mama Bite, ambaye walimsalimia tena kupitia mawasiliano ya video.
Vunjabei amesema hakufahamu kuwa muda waliokaa pamoja ungekuwa wa mwisho kwake kuwa na marehemu, akieleza masikitiko yake kwa kuondokewa na mtu aliyekuwa na nafasi muhimu katika maisha yake.
Aidha, amesema Goha alikuwa na imani kubwa katika kuwajenga vijana na kuandaa kizazi kijacho ili kiweze kupokea kijiti cha uongozi, jambo linaloonesha namna alivyothamini maendeleo ya vijana na mwendelezo wa uongozi.
Katika salamu hizo, Vunjabei ametoa pole kwa mke wa marehemu, Mama Bite, pamoja na watoto wao wanne, akiwaombea nguvu, subira na faraja katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Amesema kumbukumbu za Said Goha zitaendelea kuishi, huku akimuaga kwa salamu za mwisho na kumtakia pumziko la amani.
“Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un,”
Pumzika kwa amani, Said Goha.

