
Rubani wa Shirika la Ndege la Saudia, Kapteni Hamoud Ali AlKalthami, ameuawa katika mashambulizi yaliyolenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini humo imethibitisha kuwa uwanja huo ulilengwa na mashambulizi mawili siku ya Alhamisi, Oktoba 8, 2026, yaliyosababisha vifo vya watu watatu, akiwemo rubani huyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Saudia, shambulizi la kwanza lililenga miundombinu ya uwanja wa ndege, huku la pili likilenga ndege ya shirika hilo iliyokuwa imeegeshwa uwanjani hapo.
Shirika hilo limetoa pole kwa familia, ndugu na wafanyakazi wenzake wa rubani huyo, likieleza kuwa linatambua mchango wake katika utumishi wake kwa shirika hilo la taifa.
Aidha, shambulizi hilo lilisababisha uharibifu wa ndege hiyo, ambayo wakati wa tukio haikuwa na abiria ndani yake.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga imesema mashambulizi hayo pia yalisababisha majeruhi kadhaa, raia na wakazi wa Saudi Arabia, waliopata majeraha ya viwango tofauti, kuanzia madogo hadi makubwa. Majeruhi hao walipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, timu za dharura na vyombo husika vya usalama vilichukua hatua mara moja kukabiliana na hali hiyo na kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea.
Hata hivyo, shughuli za uwanja huo wa ndege ziliendelea kurejea katika hali ya kawaida, huku Saudia ikithibitisha kuwa safari zake za ndege katika uwanja huo zilirejea katika hali ya kawaida kuanzia saa 12:00 jioni, Oktoba 8, 2026.
Shirika hilo limeeleza kuwa linaendelea kufuatilia ratiba za safari na kutoa taarifa kwa abiria kupitia njia zake rasmi za mawasiliano.

