MBUNGE KASAKA KUGHARAMIA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO NA SITA

 

Na Matukio Daima Media ,Mbeya 

Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka, ameahidi kugharamia masomo ya kidato cha tano na sita kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lualaje wilayani Chunya watakaopata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha nne.

Kasaka ametoa ahadi hiyo katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne shuleni hapo, akiwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kunufaika na fursa za elimu na kufikia ndoto zao.

“Ninawahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika mitihani yao. Kwa watakaopata daraja la kwanza, nitagharamia masomo yao ya kidato cha tano na sita ili kuwawezesha kuendelea na elimu bila kikwazo cha gharama,” amesema Kasaka.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Mohamed Juma, amesema shule ina wanafunzi 213, lakini inakabiliwa na changamoto za miundombinu, ikiwemo uhitaji wa vyumba vya maabara na mabweni, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Pamoja na jitihada zinazofanyika, bado tunahitaji miundombinu zaidi, hususan vyumba vya maabara na mabweni, ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwawezesha wanafunzi kupata elimu katika mazingira yanayokidhi mahitaji yao,” amesema Juma.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lualaje, Leckson Mwakasuluka, amesema kata hiyo inajivunia kuwa na shule yake ya kwanza ya sekondari tangu uhuru, huku akisisitiza kuwa juhudi za kuboresha elimu zitaendelea licha ya changamoto zilizopo.

 

Mwakasuluka amesema pamoja na upungufu wa nyumba za walimu, kutokuwepo kwa uzio wa shule na uhaba wa walimu, viongozi wa kata na wadau wa elimu wataendelea kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto hizo ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

“Tunatambua changamoto zinazoikabili shule yetu, zikiwemo nyumba za walimu, uzio na uhaba wa walimu. Hata hivyo, hatutakata tamaa; tutaendelea kushirikiana na wadau pamoja na Serikali kuhakikisha changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi na shule yetu inaendelea kutoa elimu bora,” amesema Mwakasuluka.

Katika mahafali hayo, Kasaka ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya maabara, iliyokusanya shilingi milioni 35 kati ya milioni 44 zilizolengwa.

“Natoa wito kwa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi za ujenzi wa miundombinu ya shule hii, kwa sababu elimu ni msingi wa maendeleo ya watoto wetu na jamii kwa ujumla,” amesema Kasaka.