Global Publishers
October 8, 2026
1,248 views
0 Comments

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wafanyabiashara ndogo maarufu kama Machinga kutumia fursa wanazopata kukuza biashara zao na hatimaye kuwa wafanyabiashara wakubwa na walipakodi.
Chalamila amesema Serikali haiwezi kuendelea na utaratibu wa kupanga Machinga kila siku bila kuwa na mpango wa kuwawezesha kukua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Akizungumza Oktoba 7, 2026, wakati wa ziara ya kuwatembelea Machinga wanaopangwa katika Kata ya Msigani, Mbezi, Chalamila amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara hao wanatumia fursa wanazopata kama hatua ya kujikwamua kiuchumi.
Amesema Machinga wanapaswa kuichukulia biashara wanazofanya kama sehemu ya safari ya kuelekea kwenye biashara kubwa, badala ya kubaki katika kiwango cha biashara ndogo kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Chalamila amesema Machinga wanaofanya biashara katika eneo la Kariakoo wamepewa hadi Oktoba 24, 2026 kuondoka katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa shughuli zao.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuweka utaratibu mzuri wa biashara na kuhakikisha shughuli za kiuchumi jijini Dar es Salaam zinafanyika katika maeneo yaliyopangwa.
Atoa tahadhari kuhusu hali ya hewa
Chalamila pia amewataka wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, huku akisisitiza umuhimu wa kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na mamlaka husika.
Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia maelekezo yanayotolewa ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa.
Aonya kuhusu vibaka Bonyokwa
Katika ziara hiyo, Chalamila pia amewaonya wananchi wa Bonyokwa kuhusu changamoto ya vibaka na uhalifu katika maeneo hayo, akiwataka wazazi na walezi kuongeza uangalizi wa watoto wao.
Amesema watoto hawapaswi kuachwa wakitangatanga mitaani bila uangalizi, akisisitiza kuwa malezi bora yana nafasi muhimu katika kuwajenga watoto na kuwazuia kujiingiza katika makundi yanayoweza kuwapeleka kwenye vitendo vya uhalifu.
Chalamila amesema mapambano dhidi ya vibaka na uhalifu hayawezi kuachwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali yanahitaji ushirikiano kati ya familia, wananchi na serikali za mitaa.
Amesema kila upande unapaswa kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha maeneo ya Dar es Salaam yanakuwa salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani.
