Ujenzi stendi mpya Chunya kukamilika Nov.30 – HabariLeo

MBEYA;  Mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Chunya, unaojengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 30 mwaka huu.

Ujenzi wa stendi hiyo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu unatajwa kuwa chachu ya maendeleo pamoja na kivutio cha uwekezaji kwa wenyeji na wageni mbalimbali wanaofika katika wilaya hiyo.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mhandisi wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Mabasi Chunya, Mhandisi Charles Kwayi, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi makubwa 50, mabasi madogo 100, bajaji, maegesho ya magari na maduka 420 ya biashara.

“Kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi, na changamoto zilizokuwa zimejitokeza zikiwa zimeshatatuliwa na kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa mitaro na ukamilishaji wa kazi za mwisho za ujenzi,”amesema Mhandisi Kwayi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona, amesema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni mwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri,kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amealika wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali yaliyopo Chunya, akieleza kuwa kwa sasa wilaya hiyo imebadilika kutokana na maendeleo yaliyopo na ni miongoni mwa wilaya zinazopokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Amesema Halmashauri inaendelea kuboresha miundombinu kwa ajili ya wawekezaji kuja kufanya shughuli za uwekezaji na kwamba ujenzi wa miradi mbalimbali, ikiwemo uwanja wa mpira na stendi mpya, ni sehemu ya juhudi za kuweka mazingira mazuri na kuvutia watu kuja kuwekeza katika wilaya hiyo.