SERIKALI YAWAFUATILIA WAJIRI WANAOTUMIA AKAUNTI ZA WATUMISHI KUKOPA

SERIKALI imewaonya waajiri wanaotumia akaunti za watumishi wanaowasimamia kuomba mikopo binafsi bila ridhaa yao, ikisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo hivyo, ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, jijini Dodoma wakati Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ukiendesha mafunzo kwa maafisa rasilimali watu na wahasibu kutoka wizara na taasisi za umma nchini.

Mkomi amesema Serikali haijaishia kutoa onyo, bali imeanza kufuatilia mnyororo wa waajiri wanaodaiwa kujihusisha na matumizi ya akaunti za watumishi katika mikopo hiyo, ili kubaini wanaokiuka sheria na taratibu za utumishi.

Amesema kitendo cha mwajiri kutumia akaunti ya mtumishi kuomba mkopo bila ridhaa yake kinaweza kumweka mtumishi katika madhara ambayo hakuyakusudia, hivyo kinapaswa kushughulikiwa kwa uzito unaostahili.

Katika eneo la haki na ustawi wa wafanyakazi, Mkomi ameitaka WCF kutazama uwezekano wa kuongeza wigo wa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao, akitaja pia changamoto za kiafya kama shinikizo la damu.

Ameonya pia waajiri dhidi ya kuwaacha watumishi wanapolazwa hospitalini bila kuchukua hatua zinazohitajika, akiwataka kuhakikisha taarifa za hali zao zinawasilishwa katika maeneo husika ili waweze kupata msaada na stahiki zao kwa wakati.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya WCF, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Dkt. John Mduma, amesema shughuli za taasisi hiyo zina mchango katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hasa katika kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha wananchi kwa upana.

Dkt. Mduma amesema WCF inalenga kuhakiksha mfanyakazi anayepata madhara kutokana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi hapuuzwi katika safari ya maendeleo ya Taifa, bali anapata haki na huduma zinazomstahili.

Amesema ustawi, haki na usawa wa wafanyakazi ni miongoni mwa misingi inayozingatiwa na WCF katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni sehemu ya kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dkt. Mduma amesema mfuko huo utaendelea kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara yanayohusiana na mazingira ya kazi wanapata haki na huduma stahiki, ili waweze kuendelea kushiriki katika maendeleo na kunufaika na matokeo yake.