Nyumba yaanza kujengwa mama aliyeishi porini – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Nyumba mpya imeanza kujengwa kwa ajili ya mama aliyekuwa akiishi katika mazingira magumu eneo lenye pori, baada ya kuonekana akiwa kwenye mazingira magumu na kuwagusa watu mbalimbali, akiwamo Mwenyekiti wa Lake Group, mfanyabiashara na bilionea Ally Edha Awadh.

Ally alikuwa miongoni mwa wageni waliomtembelea mama huyo baada ya video yake kusambaa, ikionesha mazingira anayoishi, likiwemo nyumba yake ndogo na namna anavyojilinda dhidi ya wanyama nyakati za usiku.

Baada ya kumtembelea, Ally amesema ameguswa na hali ya maisha ya mama huyo na kuamua kuchukua hatua kwa kuanza ujenzi wa nyumba mpya kwa ajili yake.

“Nimeguswa sana na huyu bibi, kweli amenigusa moyo wangu. Sisi kama wafanyabiashara tuna wajibu wa kisheria kulipa kodi, lakini vilevile tuna wajibu wa kuwasaidia watu. Tayari nimeleta mafundi, kesho waanze,” amesema Ally.

Amesema maisha ya mama huyo yamemfundisha kuwa hata katika mazingira magumu, mtu anaweza kuendelea kuwa na matumaini na kuthamini kile kidogo alichonacho.

“Ameonyesha kwamba hakuna kitu kama matumaini na kushukuru kile kidogo ambacho anacho. Nani alitegemea tungefika pale kwenye kijumba chake na kumsalimia, halafu baada ya kipindi kifupi mama huyu atakuwa na nyumba bora?” amesema.

Ally amesema wafanyabiashara wanapofanikiwa wana wajibu wa kuwasaidia watu wenye uhitaji, akisisitiza kuwa mafanikio hayapaswi kuishia katika kulipa kodi na kutoa ajira pekee.

“Wafanyabiashara unapobarikiwa siyo tu wa kulipa kodi na kuleta ajira, bali tuna wajibu binafsi wa kuwatazama walioko chini yetu,” amesema.

Aidha, Ally amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wafanyabiashara kufanya biashara kwa wigo mpana, akisema fursa hizo zimekuwa sehemu ya kuwawezesha kufanikiwa na kuwasaidia wengine.

“Ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufanya biashara kwa uwanda mpana. Ndiyo maana unapofanikiwa tunawakumbuka walioko chini yetu. Bila Mheshimiwa Rais tusingefika tulipofika. Zamani tulikuwa tunakimbia nchi, lakini tunapopata fursa tunakuwa malaika,” amesema.

Ujenzi wa nyumba hiyo tayari umeanza, huku hatua hiyo ikitarajiwa kumbadilishia mama huyo mazingira ya maisha na kumpa makazi salama zaidi.