MENEJA Mwandamizi wa kampuni ya Palachichi International, Moses Mlowe amewataka vijana na wananchi kuingia katika kilimo cha parachichi, akisema zao hilo linaweza kuwa chanzo kizuri cha kipato kutokana zao hilo ni kuwa la muda mrefu na kuendelea kuzaa kwa miaka mingi.
Mlowe amesema ameyasema hayo leo October 7 , 3026 jijini Dodoma kwenye Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Wadau wa Tasnia ya Parachichi ambapo amesema wananchi hawapaswi kusubiri kuwa na mashamba makubwa ili kuanza kilimo hicho, bali wanaweza kuanza hata kwa idadi ndogo ya miti na kuongeza uzalishaji kadiri wanavyopata uzoefu na rasilimali.
Amesema mchakato wa kulima parachichi ni rahisi endapo mkulima atazingatia hatua muhimu tangu mwanzo, ikiwemo kuchagua eneo linalofaa na kuhakikisha udongo una afya pamoja na virutubisho vinavyohitajika.
Amesema parachichi, kama mimea mingine, huhitaji mwanga, maji na virutubisho ili kukua vizuri na kutoa mazao yenye tija, huku akisisitiza umuhimu wa mkulima kufahamu afya ya udongo kabla ya kuanza uzalishaji.
Kwa mujibu wa Mlowe, hatua nyingine muhimu ni kuchagua miche bora na kufanya upandikizaji wa kikonyo, maarufu kama upandikizaji (grafting) , ambapo mkulima huchagua aina ya parachichi anayotaka kulima kulingana na mahitaji yake.
Amesema katika uzalishaji wa miche ya parachichi, kikonyo kinapaswa kuchukuliwa kutoka kwenye mti mama wenye afya na ambao tayari umeanza kuzaa vizuri.
Mlowe amesema kutumia kikonyo kutoka kwenye mti mama unaozaa vizuri husaidia kuendeleza sifa za mti huo katika mche mpya, hivyo kumpa mkulima nafasi nzuri ya kuwa na miti yenye uwezo wa kutoa mazao bora.
” Mti wa parachichi unaweza kuanza kutoa mazao baada ya takribani miaka mitatu tangu kupandwa, huku uzalishaji ukiongezeka kadiri mti unavyokua na kuendelea kwa miaka mingi, “Amesema
Mlowe amesema mkulima anatakiwa pia kudhibiti ukuaji wa mti kwa kuupunguzausiwe mrefu usiende juu sana, jambo litakalorahisisha uvunaji na kuwawezesha hata watoto kufikia matunda wakati wa kuvuna.
Amesema mkulima mwenye miti michache anaweza kuanza kupata kipato baada ya miaka mitatu, huku uzalishaji ukiongezeka kadiri idadi ya miti inavyoongezeka na miti inavyokomaa.
Kwa upande wa kilimo cha kibiashara, Mlowe amesema kampuni yao hupanga mashamba kwa nafasi maalumu kati ya mche na mche na kati ya mstari na mstari ili kuwezesha miti kukua vizuri na kurahisisha shughuli za shamba.
” Zao la Parachichi limekuwa likijulikana kama ‘dhahabu ya kijani’ kutokana na fursa zake za kiuchumi, huku akiwahimiza wananchi kuanza hata kwa idadi ndogo ya miti kabla ya kupanua uzalishaji, ” Amesema Mlowe
Hata hivyo, amesema pamoja na fursa hizo, wakulima wa parachichi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo miundombinu ya barabara na umeme, hasa katika maeneo ya vijijini ambako mashamba mengi yanapatikana.
Amesema ukosefu wa barabara nzuri unaweza kuathiri usafirishaji wa parachichi kutoka mashambani kwenda sokoni, jambo linaloweza kusababisha matunda kuharibika kwa kuwa ni zao linalohitaji kusafirishwa kwa wakati.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa umeme vijijini umeendelea kuimarika, lakini baadhi ya mashamba yaliyo ndani zaidi bado yanahitaji nishati mbadala kama sola kwa ajili ya kusukuma maji kutoka vyanzo vya maji kwenda mashambani.
“Miundombinu bora ya barabara na umeme itasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuongeza ufanisi katika uzalishaji na biashara ya parachichi, ” Amesema Meneja huyo.
Na Kuongeza kuwa” Parachichi lina matumizi mbalimbali, likiwemo kuliwa kama tunda na kutumika kutengeneza mafuta ambayo yanaweza kutumika katika shughuli mbalimbali, hivyo kuongeza thamani ya zao hilo, ” Amesema.
Mlowe amesisitiza umuhimu wa kutumia miche bora na kufuata hatua sahihi za uzalishaji, akisema mkulima anayechagua miche na eneo vizuri, kuandaa mashimo, kupanda, kuweka maji na virutubisho pamoja na kudhibiti magonjwa na wadudu ana nafasi kubwa ya kupata mavuno mazuri.
Amesema kutokana na fursa hizo, wananchi wanaweza kuanza kilimo cha parachichi kwa kiwango kidogo na kuongeza uzalishaji kadiri wanavyopata uzoefu na rasilimali.
Mlowe ametoa wito kwa wakulima wanaotaka kuingia kwenye kilimo hicho kuzingatia uchaguzi wa miche bora, eneo linalofaa, afya ya udongo, upatikanaji wa maji na matunzo ya miti ili kuongeza tija na manufaa ya kiuchumi.
