Global Publishers
October 6, 2026
438 views
0 Comments
DAR ES SALAAM: Maandalizi ya Derby ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga yameingia hatua nyingine baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kueleza kuwa kifaa maalum cha Gas Detector kitatumika katika Uwanja wa Uhuru kufuatilia hali ya hewa na kubaini uwepo wa gesi au harufu hatarishi.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Cornel Barnabas, amesema matumizi ya kifaa hicho ni sehemu ya hatua za kuimarisha usalama wa mashabiki na wadau watakaohudhuria mchezo huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 10, 2026.
Barnabas amesema pamoja na hatua hizo za usalama, mchezo huo utatumia utaratibu maalum wa FVS, ambapo benchi la kila timu litapewa kadi mbili za kuomba tukio liangaliwe kupitia mfumo huo.
Amesema jumla ya kadi nne zitatumika katika mchezo huo, huku kila benchi likiwa na kadi zake mbili.
Kwa mujibu wa Barnabas, endapo benchi litaona kuwa kuna tukio ambalo linahitaji msaada wa FVS ili kuhakikisha haki inatendeka, litapaswa kuinua kadi yake kuomba mwamuzi akague tukio hilo kupitia mfumo huo.
Hata hivyo, amesema ombi hilo linapaswa kufanyika ndani ya sekunde 60 tangu tukio litokee, na benchi halitaruhusiwa kusubiri hadi tukio lipite ndipo kuwasilisha ombi la kutumia FVS.
“Sharti ni kwamba benchi linatakiwa kuonesha kadi yao juu ndani ya sekunde 60, haitakiwi kuchelewa hadi tukio lipite,” amesema Barnabas.
Derby hiyo ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga imepangwa kuchezwa Oktoba 10, 2026 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku maandalizi ya usalama na matumizi ya teknolojia yakilenga kuhakikisha mchezo unafanyika katika mazingira salama na yenye usimamizi wa karibu.

