Kikwete Akutana na Guterres New York Kujadili Amani Sudan Kusini

Global Publishers
October 6, 2026
474 views
0 Comments

NEW YORK: Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika muktadha wa majukumu ya Dkt. Kikwete kama Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kuhusu Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili pia juhudi za kuendeleza amani na utulivu nchini Sudan Kusini.

Mkutano huo umefanyika wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea katika kutafuta suluhu za changamoto za amani na usalama katika eneo la Pembe ya Afrika na Sudan Kusini.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Togolani Mavura.