Watuhumiwa 11 Wakamatwa Kwa Tuhuma za Wizi Kwa Njia Ya Mtandao

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 11 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kifedha kupitia makundi ya mitandao ya kijamii, huku likiendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika mtandao huo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao wanadaiwa kutumia makundi ya WhatsApp na Instagram yanayojulikana kwa majina ya C2203 VDC Dawn, VBCL Business Company Ltd, Fine Modern Homes na Fine Group of Companies kuwalaghai wananchi.

Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya uhalifu huo kwa kujitambulisha kuwa kampuni hizo zinaendeshwa na Prof. Vicent Mwakatobe, Rebeka Mponzi na Andrew Komba.

Jeshi hilo limeeleza kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakitoa matangazo yenye viunganishi maalum (links), ambavyo watu wanapoingia hudaiwa kupewa maelekezo ya kufanya malipo kupitia akaunti mbalimbali kwa lengo la kununua hisa katika masoko ya hisa ikiwemo Dar es Salaam Stock Exchange (DSE), London Stock Exchange na masoko ya Marekani, au kulipia huduma za ujenzi wa nyumba.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi linadai kuwa miamala hiyo imekuwa ikifanyika kupitia mikataba hewa, hali inayosababisha wananchi kupoteza fedha zao.

Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo sambamba na kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa, wakiwemo watu wanaodaiwa kuwa wapiga debe wanaohamasisha wananchi kujiunga na shughuli hizo kwa kuwashawishi kuwa ni biashara halali.

Jeshi la Polisi limesema vitendo hivyo vinadaiwa kuwa sehemu ya uhalifu wa kimtandao unaolenga kuwaibia wananchi kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na kampuni zinazotangaza fursa za uwekezaji au biashara kupitia mitandao ya kijamii, na kuwataka kufanya uhakiki wa kina kabla ya kutoa fedha au kuingia katika mikataba.

Aidha, wananchi wametakiwa kuthibitisha uhalali wa kampuni na shughuli zake kupitia mamlaka husika zinazohusika na usajili na udhibiti wa biashara na uwekezaji, ili kuepuka kuingia katika mitego ya utapeli wa mtandaoni.