WANANCHI LIWALE NA NACHINGWEA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA JITIHADA ZA KUDHIBITI UVAMIZI WA NDOVU

LINDI

WANANCHI wa Wilaya za Liwale na Nachingwea mkoani Lindi wameiomba Serikali kuongeza jitihada za kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, hususan Ndovu, wanaovamia mashamba na maeneo ya makazi, kuharibu mazao, kujeruhi na wakati mwingine kusababisha vifo.

Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa jumla ya hekari 52,624.24 za mashamba ya wananchi zimeathiriwa na uvamizi wa tembo, huku wananchi 4,709 wakikumbwa na madhara hayo.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo katika maeneo tofauti mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, aliyefika kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na uvamizi wa tembo.

Katika Kata ya Kiangara wilayani Liwale na Kipala Mnelo wilayani Nachingwea, wananchi wameeleza kuwa hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo, ikiwemo uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Mbali na kupunguza uzalishaji, wananchi wamesema uvamizi huo umekuwa ukiwafanya waishi kwa hofu kutokana na uwepo wa Ndovu katika mashamba na maeneo ya makazi.

Wakizungumza katika maeneo hayo, wananchi wameiomba Serikali kuongeza nguvu katika kudhibiti wanyama hao, ili kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao unalindwa, sambamba na kuwawezesha kuendelea na shughuli za kilimo bila hofu.

Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, amesema Serikali inatambua changamoto ya uvamizi wa Ndovu inayowakabili wananchi na tayari imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo.

Naibu Waziri Chande amesema Serikali itaendelea kusimamia hatua zinazolenga kupunguza madhara yanayotokana na wanyama hao, huku ikitafuta njia zitakazowezesha wananchi kuishi na kufanya shughuli zao kwa usalama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, ameeleza kuwa uvamizi wa Ndovu ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya wananchi na kwa ujumla kurudisha nyuma juhudi za maendeleo ya Mkoa wa Lindi.

Amesema uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyama hao unaathiri uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara, hivyo ni muhimu hatua zaidi kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanalindwa na wanaendelea kuzalisha kwa tija.