Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuwa jumla ya wanafunzi 4,213,144 watafanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, Darasa la Nne na Kidato cha Pili utakaofanyika katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea Zanzibar mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Octoba 4,2026 Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed amesema, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026 katika shule za msingi 21,008, huku wanafunzi 1,591,064 wakitarajiwa kushiriki.
Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili ngazi ya shule utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026 katika shule za msingi 21,353, ambapo wanafunzi 1,827,367 wamesajiliwa, wakiwemo wavulana 906,545 na wasichana 920,822.
Kwa upande wa Kidato cha Pili, amesema wanafunzi 794,713 wamesajiliwa kufanya upimaji huo utakaofanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026 katika shule za sekondari 6,612 pamoja na vituo 599 vya watahiniwa wa kujitegemea Tanzania Bara na Zanzibar.
Profesa Mohamed amesema kati ya wanafunzi wa Kidato cha Pili waliosajiliwa, 786,163 ni wanafunzi wa shule, huku 8,550 wakiwa watahiniwa wa kujitegemea, ambapo wasichana wa shule ni 434,627 sawa na asilimia 55.28 dhidi ya wavulana 351,536 sawa na asilimia 44.72.
Amesema katika Darasa la Pili, wanafunzi 1,675,355 sawa na asilimia 91.68 watafanya upimaji kwa Kiswahili, huku 152,012 sawa na asilimia 8.32 wakifanya kwa Kiingereza kulingana na lugha wanayotumia katika kujifunza.
Kwa Darasa la Nne, wanafunzi 1,468,885 sawa na asilimia 92.32 watafanya upimaji kwa Kiswahili, wakati 122,179 sawa na asilimia 7.68 watafanya kwa Kiingereza, huku wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa 5,603.
Amesema pia wanafunzi 5,295 wa Darasa la Pili wenye mahitaji maalum wamesajiliwa, wakiwemo wenye uoni hafifu 1,062, wasioona 112, wenye uziwi 929, ulemavu wa akili 1,208 na ulemavu wa viungo 1,984.
Kwa Kidato cha Pili, wanafunzi 781,127 watafanya upimaji katika Mkondo wa Jumla, huku 5,036 wakifanya katika Mkondo wa Amali, unaotahiniwa kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023.
Aidha Profesa Mohamed amesema maandalizi ya upimaji huo yamekamilika, ikiwemo kusambazwa kwa karatasi za upimaji na nyaraka muhimu katika Halmashauri na Manispaa, huku maandalizi maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum yakifanyika.
Ameonya wanafunzi dhidi ya vitendo vya udanganyifu, akisema yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu atafutiwa matokeo kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani, huku wasimamizi wakitakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki yake.
Aidha, NECTA imewataka wamiliki na wakuu wa shule kutoingilia majukumu ya wasimamizi wa upimaji na imeonya kuwa kituo chochote kinaweza kufutwa endapo usalama wa upimaji utahatarishwa. Jamii nayo imetakiwa kutoa ushirikiano na kutoa taarifa za udanganyifu kupitia namba 0759360000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz.
