ARUSHA: WAFANYABIASHARA wa bidhaa za asili jijini Arusha wameeleza kuwa ujio wa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ni fursa kubwa ya kutangaza na kuuza bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Mfanyabiashara wa bidhaa za asili, Happy Mlinga, amesema leo kuwa ujio wa wageni hao umeongeza matumaini kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na bidhaa za utamaduni na sanaa za Tanzania.

Amesema wafanyabiashara hao wana bidhaa mbalimbali zikiwemo mavazi, mashati, bidhaa za ngozi, kazi za mikono pamoja na sanaa zinazobeba utamaduni wa Tanzania.
“Tunashukuru sana kwa ugeni huu mkubwa tunaouona. Tunaamini ni fursa kwetu kwa sababu tuna bidhaa nzuri, zikiwemo maguni, mashati, bidhaa za asili na kazi mbalimbali za mikono,” amesema Mlinga.
Alisema wageni wanaofika nchini wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea maeneo yanayouza bidhaa za asili ili kujionea ubora wa bidhaa zinazotengenezwa na Watanzania
Mlinga amesema bidhaa hizo ni sehemu ya utambulisho wa Tanzania na kwamba ununuzi wake unasaidia kuongeza kipato kwa wafanyabiashara na wasanii wanaozalisha bidhaa hizo.

“Karibuni sana muone bidhaa za Tanzania. Hizi ni bidhaa halisi na original, tunawaomba wageni wasikose fursa ya kuziona na kununua bidhaa zetu,” amesema
Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9 huku ukiwakutanisha wabunge na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani, hali inayotarajiwa kuongeza fursa za biashara, utalii na kutangaza bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa
