Chivayo na Mkewe Kuzikwa Pamoja Oktoba 8 Glen Forest, Harare

Global Publishers
October 4, 2026
0 views
0 Comments

HARARE, Zimbabwe — Mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mkewe Lucy Muteke ‘Lulu’, wanatarajiwa kuzikwa pamoja siku ya Alhamisi, Oktoba 8, katika Makaburi ya Glen Forest jijini Harare.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia za Chivayo na Muteke, mazishi hayo yatafanyika kuanzia saa 8:00 mchana.

Familia hizo zilisema zinaendelea kuwa pamoja katika kipindi hiki cha majonzi kufuatia kifo cha wanandoa hao, ambao walifariki katika ajali ya helikopta iliyotokea Marondera wiki iliyopita.

“Wicknell alikuwa fahari yetu mtu mwenye maono, imani na ukarimu usio na kifani. Lulu alikuwa furaha yetu mtu mpole na mwenye upendo. Walipendana kwa dhati na wanaondoka pamoja,” familia hizo zilisema katika taarifa ya msiba.

Familia hizo pia zimewashukuru wananchi wa Zimbabwe kwa kuwaunga mkono na kuwafariji tangu kutokea kwa msiba huo.

Chivayo, mwenye umri wa miaka 46, na Muteke, mwenye umri wa miaka 35, walifariki Septemba 30 baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Kudenga Farm, Marondera.

Katika ajali hiyo, watu wengine watatu pia walipoteza maisha. Waliotajwa ni rubani Calvin Tafirei Soda, rubani msaidizi Courage Mutavirwa na mlinzi Saneliswe Magagula.

Mazishi ya wanandoa hao yanatarajiwa kuwakutanisha ndugu, marafiki na waombolezaji katika kuwaaga kwa mara ya mwisho.