Global Publishers
October 2, 2026
36 views
0 Comments
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limemkamata Faustine Zakaria, kwa tuhuma za kuharibu fedha halali za Tanzania baada ya picha zake akifanya vitendo hivyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Jeshi hilo limeeleza kuwa Faustine alionekana katika picha akizitawanya sakafuni noti za Tanzania pamoja na nyele zilizotokana na shughuli za unyoaji na uchafu mwingine ndani ya saluni yake.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa alirekodiwa kwa ridhaa yake huku akifahamu kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria. Baada ya kurekodi video hiyo, aliisambaza kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii Agosti 23, 2026.
Hatua hiyo iliwezesha mamlaka za kisheria kufuatilia tukio hilo na kuchukua hatua stahiki.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku mtuhumiwa akitarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuheshimu, kulinda na kutunza fedha za Tanzania, likisisitiza kuwa fedha hizo ni alama ya utambulisho na heshima ya taifa.
Aidha, wananchi wametakiwa kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kudhalilisha au kuharibu fedha hizo.


