Mloganzila yalaza wagonjwa watano wa kiharusi kila siku – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila hulaza wagonjwa kati ya watano na saba wenye kiharusi kila siku, hali inayodhihirisha ukubwa wa tatizo hilo na umuhimu wa jamii kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo.

Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka hospitalini hapo, Dk Brighton Mushengezi, amesema kiharusi kinaendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya duniani na hutokea pale mzunguko wa damu kwenda kwenye ubongo unapozuiwa au mshipa wa damu katika ubongo unapopasuka.

Amesema hali hiyo husababisha sehemu ya ubongo kukosa oksijeni na virutubisho vinavyohitajika, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa mgonjwa endapo hatapatiwa huduma kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dk Mushengezi, dalili za kiharusi zinaweza kujitokeza ghafla na ni pamoja na uso kupinda upande mmoja, mkono au mguu kuwa dhaifu au kufa ganzi, kushindwa kuzungumza au kuelewa mazungumzo, kupoteza uwezo wa kuona pamoja na kushindwa kutembea vizuri.

Amesema takwimu za Shirika la Kiharusi Duniani (World Stroke Organization) za mwaka 2025 zinaonesha kuwa takribani watu milioni 12 hupata kiharusi kila mwaka duniani.

Ameongeza kuwa shirika hilo linaeleza pia kuwa mtu mmoja kati ya watu wanne wenye umri wa miaka 25 na kuendelea yuko katika hatari ya kupata kiharusi katika maisha yake, hali inayosisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa wa ugonjwa huo na kuchukua hatua za kinga.

Dk Mushengezi ametaja shinikizo la damu kuwa miongoni mwa vihatarishi vikubwa vya kiharusi, huku kisukari, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa na matumizi hatarishi ya pombe pia vikiongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

Amesema baadhi ya vihatarishi hivyo vinaweza kudhibitiwa kwa kubadili mtindo wa maisha, ikiwamo kufanya mazoezi, kula mlo unaofaa, kudhibiti shinikizo la damu na kisukari pamoja na kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kwa kiwango hatarishi.

Aidha, amewataka wananchi kutopuuza dalili za kiharusi zinapojitokeza, bali kuwahi kumfikisha mgonjwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Amesema utambuzi na matibabu ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na kiharusi, huku elimu kwa jamii kuhusu dalili, vihatarishi na hatua za kuchukua ikiwa muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo.