SERIKALI YAWEKA MKAKATI MAALUM KWA WATU WENYE ULEMAVU WAKATI WA EL NIÑO

 

Na Matukio DaimaMedia 

Serikali imeweka mkakati maalum wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata taarifa kwa wakati kuhusu mvua za El Niño pamoja na hatua za kuchukua kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwamo kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia kulingana na mahitaji yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema mbinu na nyenzo maalum tayari zimeandaliwa kwa ajili ya kutoa taarifa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu, yakiwamo watu wenye uoni hafifu, viziwi na wenye ulemavu wa aina nyingine.

Profesa Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika Jukwaa la Uratibu na Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki na Ustawi wa Watu Wenye Ualbino Bandiliko wa mwaka 2024–2029, lililowakutanisha wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa mpango huo.

Amesema maandalizi hayo ni sehemu ya kuhakikisha makundi yenye mahitaji maalum hayaachwi nyuma wakati wa utoaji wa taarifa za tahadhari, hasa katika kipindi ambacho Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño.

Akizungumzia hali ya ulinzi na haki za watu wenye ualbino bandiliko, Profesa Kabudi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili kundi hilo, ikiwamo unyanyapaa, ubaguzi, mauaji na vitendo vya ukatili.

Kwa upande wao, wawakilishi wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) wameipongeza Serikali kwa juhudi zinazochukuliwa katika kupambana na mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, wakisema utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa unatoa matumaini ya kuboresha zaidi maisha yao.

Wamesema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuendelea kufungua fursa sawa kwa watu wenye ualbino katika maeneo muhimu kama elimu, ajira na huduma za afya, huku ukisaidia kuimarisha ulinzi wa haki zao na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi, hatua inayolenga kuboresha huduma na mazingira ya watu wenye ulemavu nchini.

Jukwaa hilo limewakutanisha wawakilishi wa Serikali, taasisi za kimataifa, asasi za kiraia pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuimarisha uratibu wa hatua zinazolenga kulinda haki, usalama na ustawi wa watu wenye ulemavu nchini

.