
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Septemba 29, 2026, inatarajiwa kuanza kusikiliza mawasilisho ya mwisho ya upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu .
Mawasilisho hayo yanatarajiwa kuwasilishwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, baada ya Lissu kukamilisha mawasilisho yake ya mwisho jana, Septemba 28, mbele ya jopo la majaji watatu.
Kesi hiyo, yenye namba 19605/2025, inasikilizwa na jopo linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Katika mawasilisho yake, Lissu aliiomba Mahakama kuangalia kama upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kosa linalomkabili kwa kiwango kinachotakiwa katika kesi za jinai, yaani bila kuacha shaka yenye msingi.
Lissu pia alitoa kauli kwamba iwapo majaji wataona kuwa kosa la uhaini limethibitishwa, watoe hukumu kwa mujibu wa sheria, na iwapo hawatabaini kuwa kosa hilo limethibitishwa, wamwachie huru.
Katika hoja zake, Lissu alipinga kwa kina ushahidi wa upande wa Jamhuri, akiwemo ushahidi kuhusu mkutano wa Aprili 3, 2025, tafsiri ya maneno anayodaiwa kuyasema, pamoja na hoja kuhusu kama maneno hayo yanaweza kisheria kuunda kosa la uhaini.
Baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha mawasilisho yake, hatua inayofuata itakuwa Mahakama kutathmini hoja na ushahidi uliowasilishwa na pande zote kabla ya kutoa uamuzi kwa mujibu wa sheria.
