MABAHARIA WA TANZANIA WAGEUKA MABALOZI WA UTALII, NGORONGORO YAWAPA SABABU YA KUHAMASISHA DUNIA

Na Matukio Daima Media, Arusha

KATIBU wa Jumuiya ya Mabaharia Tanzania (Old Navy), Daniel Masele, amewataka Watanzania kuacha kuangalia hifadhi na vivutio vya utalii kama vitu vya wageni pekee, akisema safari yao katika Bonde la Ngorongoro imewapa fursa ya kushuhudia kwa macho yao utajiri wa asili ambao Tanzania imejaaliwa.

Masele amesema mabaharia hao, ambao wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali duniani, wamekutana na mambo mengi katika safari zao, lakini baadhi ya yale waliyoyaona, Tanzania ni ya kipekee na hawajawahi kuyaona katika maeneo mengine waliyofika..

Amesema walipokuwa Ngorongoro walishuhudia wanyama mbalimbali wanaoishi ndani ya kreta, jambo alilolitaja kuwa sehemu ya maajabu yanayopaswa kuwafanya Watanzania wenyewe kuwa sehemu ya kwanza ya kutembelea na kuitangaza nchi yao.

Kwa mujibu wa Masele, Tanzania imekuwa ikipata mapato kupitia utalii, huku sehemu kubwa ya wageni wanaotembelea vivutio hivyo wakitoka nje ya nchi, hivyo Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kuvifahamu vivutio vyao na kuwa mabalozi wa utalii wanapokwenda maeneo mbalimbali.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mohamed Said Ngamba, ambaye amesema wazo la kuanzisha Old Navy lilitokana pia na kutambua nafasi waliyonayo mabaharia kuitangaza Tanzania kutokana na mazingira yao ya kazi yanayowapeleka katika nchi na maeneo mbalimbali duniani.

Ngamba amesema wakiwa safarini baharini walikuwa wakifuatilia juhudi mbalimbali za kuitangaza Tanzania, ikiwemo kupitia Royal Tour, na kuona kuwa nao wana wajibu wa kushiriki katika kuitangaza nchi yao na kumuunga Mkono Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kueleza kwa watu wanaokutana nao kuhusu vivutio vilivyopo Tanzania.

Amesema mabaharia ni sehemu ya wawakilishi wanaokutana na watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo Jumuiya yao imeamua kutumia nafasi hiyo kuhamasisha utalii kwa ushuhuda wa maeneo wanayoyatembelea wenyewe.

“Hatupaswi kukaa kimya wakati nchi yetu ina vivutio vingi. Kama tunasafiri na kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, tunapaswa kuwaambia Tanzania ina nini na kuwaalika waje kuona wenyewe,” amesema Ngamba.

Ameeleza kuwa ziara ya Ngorongoro ni sehemu ya mpango wao wa kutembelea vivutio mbalimbali nchini, wakianza na Mikumi na baadaye kutembelea maeneo mengine, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, ili wanapozungumza kuhusu utalii wa Tanzania wawe wameviona vivutio hivyo kwa macho yao.

Amesema katika ziara hiyo amevutiwa na mandhari ya Ngorongoro pamoja na wanyama mbalimbali aliowaona, akiwemo Simba, Faru, Pundamilia na Kiboko, na kwamba uzoefu huo utawapa nguvu zaidi katika kuwahamasisha wengine kutembelea Tanzania.

Mabaharia wengine walioshiriki ziara hiyo, Omary Said Kipelele, Siwatu Hassan Sembi, Fahad Mohamed na Miraji Omary, wamesema watatumia fursa walizonazo kuwahamasisha ndugu, marafiki na watu wanaokutana nao nje ya Tanzania kutembelea nchi hiyo na kushuhudia vivutio vilivyopo.

Wamesema wanatambua umuhimu wa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza sekta ya utalii, huku wakimshukuru Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt Mahmoud Thabit Kombo, kwa kusaidia kuwezesha safari zao za kutembelea hifadhi za Taifa ili waweze kupata uzoefu wa moja kwa moja wa vivutio wanavyotaka kuvitangaza.

Kwa upande wake, mdau wa utalii kutoka Kampuni ya Utalii ya Mbapari, Isaya John, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea hifadhi kwa kuwa gharama za kuingia kwa raia wa Tanzania zimewekwa katika viwango vinavyoweza kumudu, hivyo wananchi hawapaswi kuziacha fursa hizo na kuwaachia wageni pekee.

Wito huo umejitokeza pia wakati zaidi ya watu 1,700 waliokuwa wakishiriki Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL Week 2026), iliyofanyika Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha, baadhi yao walipopata fursa ya kutembelea Ngorongoro na wengine vivutio vingine Jijini humo.

Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Yasin Msangi, amesema washiriki hao walikuwa wamekutana Arusha kwa ajili ya wiki hiyo iliyofanyika Septemba 22 hadi 26, 2026, na kuvutiwa kutumia nafasi hiyo ambapo watu zaidi ya 1000 wakiwa na magari zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakaamua kutembelea Ngorongoro na kujionea vivutio vilivyopo.

Msangi amesema ziara hiyo imewapa washiriki fursa ya kuona kwa vitendo kile ambacho mara nyingi hukisikia au kukisoma, huku akiwataka Watanzania wengine kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi na vivutio vya ndani

Kwa upande wao, Mabaharia wa Tanzania wamesema safari yao haitakuwa ya mara moja, bali wanatarajia kuendelea kutembelea maeneo mengine ya utalii nchini na kutumia uzoefu huo kuwaeleza wengine, hasa wanaokutana nao katika safari zao za kimataifa, kuhusu uzuri na utajiri wa Tanzania.