GEITA: WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewaomba wafanyabiashara, wajasiriamali na wachimbaji wadogo kuzingatia usajili wa nembo ya biashara badala ya kuishia kusajili jina la biashara pekee.
Ofisa Usajili BRELA, Athumani Makuka ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika badala la BRELA kwenye viwanja vya Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.
Makuka amesema watanzania wanapaswa kutambua kuwa BRELA inatoa huduma nyingi na siyo usajili wa majina ya makampuni pekee ambapo huduma zote zinaambatana na usajili ili kutoa haki miliki.
Amesema usajili wa nembo ya biashara ni muhimu kwa kila mfanyabiashara ama mchimbaji mdogo mwenye taasisi ama kampuni ili kumsaidia kutumia nembo hiyo kama mbadala wa jina la kampuni.
Amesema hatua zote za usajili zinamsaidia mhusika kuwa na uhalali wa matumizi ya nembo ya biashara pasipo kikwazo na kuzuia nembo hiyo kutumika vibaya na watu wengine bila taarifa ya mwaasisi.
“Usajili una umuhimu katika kusaidia maendeleo ya mfanyabiashara kwani ukitaka Kwenda benki kuomba mkopo utalizwa kama tayari umesajili BRELA na hata ukiomba zabuni inahitaji usajili wa BRELA.

“Pia kuanzisha biashara bila usajili kuna hatari kubwa ya kuziwa kwa maana mtu anaweza akaja akasajili baadaye wewe ambaye ulianzisha kwa kutumia nguvu nyingi mwisho wa siku ukapokonywa jina la biashara”, amesema Makuka.
Amesema usajili wa makampuni katika mfumo wa BRELA inarahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi kitaifa juu ya kampuni au taasisi zinazojihusisha na sekta fulani ikiwemo sekta ya madini.
