WAONYWA KUWAPELEKA MIKOANI DARASA LA SABA 2026 KABLA YA MATOKEO ‎

 

‎

‎Wazazi, walezi na jamii wametakiwa kuwa na tahadhari ya kuwapeleka Jijini Dar es Salaam na mikoa mingine mikubwa wahitimu wa Darasa la Saba wa mwaka huu, kabla ya kutangazwa matokeo ya kitaifa, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha baadhi yao kushindwa kujiunga Kidato cha Kwanza Januari 2027. 

‎Wito huo umetolewa na wananchi wa Kijiji cha Samamba, Kata ya Kituntu, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, wakati wa mahafali ya nne ya Shule ya Msingi Samamba, iliyoshika nafasi ya kwanza kimkoa kwa miaka mitatu mfululizo.

‎Aidha Wananchi hao wameitaka jamii kutambua na kuunga mkono juhudi za walimu wanapofanya kazi kwenye mazingira magumu, yenye changamoto, ikiwemo kuwapa pongezi na motisha wanapofanya vizuri, ili kuongeza bidii na ari zaidi ya kuendelea kuboresha ufaulu wa wanafunzi.

‎Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samamba, Adinani Mkuki, ameeleza mambo mbalimbali yanayochangia mafanikio ya shule hiyo katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kwa kutaja ushirikiano baina ya wazazi, walimu na serikali kama silaha kuu ya mafanikio.

‎Diwani wa Kata ya Kituntu, Ali Ramadhani, ametoa tahadhari kuhusu watu wanaowarubuni wanafunzi, hususan wasichana, kwa ahadi za kuwapeleka mijini au mikoani kwenda kufanya kazi za ndani kabla ya matokeo. Naye mwakilishi wa benki ya NMB Tawi la Singida Mjini,Chimlumbe Wenda,ametaka wazazi na walezi kushirikiana kuwalinda wahitimu hao, dhidi ya vishawishi hivyo.

‎Kwa upande wao, wahitimu wa Darasa la Saba akiwemo Amosi Masanja ameeleza kuwa pamoja na kufanya vizuri kitaaluma, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa.

‎Shule ya Msingi Samamba ilianzishwa mwaka 2014 kwa nguvu za wazazi na sasa ina wanafunzi 666, wakiwemo wasichana 334, pamoja na walimu 11, lakini kutokana na upungufu wa walimu, wazazi wamekuwa wakigharamia posho za walimu watatu wa kujitolea ili wanafunzi waendelee kupata huduma bora ya elimu bila kukwama.

‎