Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuimarisha ushiriki wa wananchi katika matengenezo ya barabara kupitia Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM) unaolenga kulinda miundombinu ya barabara huku ukifungua fursa za ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
Akizungumza pembezoni mwa Mkutano wa Mwaka wa Wahandisi uliofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mratibu wa mpango wa CBRM TARURA, Mhandisi Richard Missa amesema mpango huo unatekelezwa chini ya mradi wa RISE unaogharamiwa na fedha za mapato ya ndani ya Serikali Tanzania na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ukiwa na muda wa utekelezaji wa miaka mitatu.
Amesema kupitia mpango huo wananchi wanaoishi jirani na barabara huunganishwa katika vikundi vya kijamii na kupewa mikataba ya kufanya kazi za matengenezo ya kawaida ya mara kwa mara hatua inayowawezesha kushiriki moja kwa moja katika utunzaji wa miundombinu inayowahudumia kila siku.
”Lengo ni kuhakikisha barabara zinabaki katika hali nzuri kwa muda mrefu huku wananchi wanaoishi karibu na barabara wakipata fursa ya ajira na kuongeza kipato”, amesema Mhandisi Missa.
Ameeleza kuwa miongoni mwa kazi zinazotekelezwa na vikundi hivyo ni kuzibua na kusafisha mifereji na makalavati, kusafisha madaraja, kufyeka nyasi kandokando ya barabara, kuondoa magogo na miti iliyoanguka pamoja na kurekebisha au kuweka alama za barabarani zilizoanguka.
Kwa mujibu wa Mhandisi Missa, utekelezaji wa kazi hizo kwa wakati unasaidia kuzuia maji ya mvua kutuama au kuharibu barabara kwa kuhakikisha mifereji, makalavati na maeneo ya kupitisha maji yanakuwa wazi na kupelekea miundombinu ya barabara kufanya kazi kwa ufanisi haswa wakati wa mvua.
Amesema mpango huo tayari umeanza kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini ambapo zaidi ya kilomita 1,500 za barabara zimeanza kufanyiwa matengenezo kupitia vikundi 302 katika mikoa ya Tanga(Lushoto, Korogwe, Pangani), Morogoro (Mvomero, Kilombero), Pwani (Rufiji, Mkuranga) na Dodoma (Kongwa).
Akieleza hatua inayofuata, Mhandisi Missa amesema katika mwaka wa fedha 2026/27 mpango huo unatarajiwa kufikia utekelezaji wa zaidi ya kilomita 7,293 za barabara katika mikoa 25 na halmashauri za wilaya zaidi ya 104 kati ya 184 nchini.
Amesema TARURA pia ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kutoa mikataba kwa zaidi ya vikundi 1,400 ambapo kila kikundi kinatarajiwa kuwa na wanachama kati ya 5 hadi 20.
Ameeleza kuwa mpango wa CBRM unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya matengenezo ya kawaida ya barabara huku wananchi wakishiriki moja kwa moja katika kuhakikisha miundombinu inatunzwa, inapitika na inadumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Mpango wa CBRM ni hatua kubwa inayofanywa na serikali kupitia TARURA katika kuhakikisha sheria ya Ununuzi ya Umma inayoelekeza fedha za maendeleo 30% zitumike kwa kuwanufaisha wananchi kupitia ushiriki wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Aidha, ushiriki wa wananchi kupitia CBRM unatoa fursa kwa jamii kutumia rasilimali na nguvu kazi iliyopo katika maeneo yao huku TARURA ikiendelea kuimarisha ubora na usalama wa mtandao wa barabara nchini.
