TBS yasisitiza upimaji bidhaa za ujenzi – HabariLeo

DAR ES SaLAAM: SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewasihi wahandisi na watumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi kutumia huduma ya Upimaji wa Hiari (Type Testing) ili kujiridhisha kuhusu ubora wa bidhaa hizo kabla ya kuzitumia katika miradi ya ujenzi.

Wito huo umetolewa na Yona Afrika wa TBS wakati wa Maonesho ya Wahandisi yaliyofanyika Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo alieleza kuwa ubora wa bidhaa na malighafi za ujenzi ni msingi muhimu wa kuhakikisha usalama, uimara na ustahimilivu wa majengo na miradi mbalimbali.

Alisema TBS inatoa huduma ya Upimaji wa Hiari (Type Testing – TT) inayowawezesha wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na watumiaji kujiridhisha kuhusu ubora na utendaji wa bidhaa na malighafi mbalimbali kabla ya matumizi.

Kwa mujibu wa Yona, huduma hiyo inafanywa na wataalamu wenye weledi kwa kutumia maabara zenye vifaa na mitambo maalumu, huku vipimo vikizingatia viwango na taratibu zinazotambulika kitaifa na kimataifa.

Alisema matokeo ya vipimo husaidia kutoa taarifa muhimu kuhusu sifa na utendaji wa bidhaa au malighafi zinazokusudiwa kutumika, hatua inayoweza kusaidia watumiaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuanza matumizi.

TBS imewataka watumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi kuchukua hatua mapema kwa kupima bidhaa hizo badala ya kusubiri changamoto za ubora kujitokeza baada ya matumizi.

“Usisubiri changamoto ijitokeze ndipo uchukue hatua. Kama wewe ni mtumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi, fika TBS na tumia huduma ya Type Testing ili kujiridhisha kuhusu ubora kabla ya matumizi,” alisema.

Huduma hiyo inalenga kuongeza uelewa na matumizi ya bidhaa zinazokidhi viwango, hivyo kuchangia katika ujenzi wa majengo na miradi yenye usalama, uimara na ubora unaokubalika.