
Msanii wa Tanzania, Rayvanny, ametangazwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha kubwa la Afro Nation Portugal 2027, nchini Ureno.
Jina la Rayvanny limeonekana katika orodha ya kwanza ya wasanii iliyotangazwa na waandaaji wa tamasha hilo Septemba 23, 2026, hatua inayomweka tena msanii huyo wa Tanzania kwenye jukwaa kubwa la muziki wa Afrika kimataifa.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 9 hadi 11, 2027, katika ufukwe wa Praia da Rocha, Portimão, nchini Portugal, likiwa na lengo la kuunganisha muziki, utamaduni na burudani kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani.
Rayvanny atashiriki jukwaa hilo pamoja na baadhi ya majina makubwa katika muziki wa Afrika na kimataifa, akiwemo Davido, Rema, Fally Ipupa, Omah Lay, Victony na Shenseea.
Davido, Rema na Fally Ipupa wametajwa miongoni mwa wasanii wakuu watakaotumbuiza katika tamasha hilo.
Kwa upande wa muziki wa Amapiano, jukwaa la Piano People Stage linatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali, akiwemo Kabza De Small, TxC na Dlala Thukzin.
Waandaaji wa Afro Nation wamesema orodha hiyo bado haijakamilika, huku wasanii wengine wakitarajiwa kutangazwa katika awamu zijazo kuelekea tamasha hilo.
Kwa Rayvanny ushiriki huo unampa nafasi ya kuwakilisha muziki wa Tanzania katika moja ya matukio ya kimataifa yanayolenga Afrobeats, Amapiano na muziki wa Afrika. Tamasha hilo limekuwa likifanyika Portugal tangu mwaka 2019 na limeendelea kuwaleta pamoja wasanii na mashabiki kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Na Anifa Mwegelo
