Rais Samia Aunganisha Dunia Kwenye Ajenda ya Afya ya Mama na Mtot

NEW YORK, Marekani — Septemba 25, 2026 Viongozi na wadau wa afya duniani wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuimarisha afya ya mama na mtoto, huku wakisisitiza umuhimu wa wanawake kushirikishwa zaidi katika uongozi na maamuzi ya mifumo ya afya.

Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndeitwah, amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda afya na utu wa wanawake na watoto ina umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa Afrika.

Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu wenye kaulimbiu “Advocacy for a New Era: Women Leading Maternal and Child Health for All”, maarufu kama SHE RISES, Rais Nandi-Ndeitwah amesema uwekezaji katika afya ya mama na mtoto haupaswi kuonekana kama matumizi ya kawaida, bali ni uwekezaji katika watu, uchumi na maendeleo endelevu.

Mkutano huo umeandaliwa na Rais Samia, ambaye anahudumu kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika New York, Marekani.

Rais wa Namibia amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwezo wao wa ndani wa kugharamia huduma za afya ya mama na mtoto badala ya kutegemea zaidi misaada kutoka nje.

Amesema maendeleo ya Bara la Afrika hayawezi kutenganishwa na afya ya wananchi wake, huku Namibia ikiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa ajenda hiyo ya Umoja wa Afrika.

Tanzania Yaonyesha Mafanikio

Akiwasilisha uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema uwekezaji katika sekta ya afya umeanza kuonyesha matokeo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika mkutano huo, kati ya mwaka 2015 na 2022, vifo vya uzazi vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

Aidha, bajeti ya afya imeongezeka kutoka takribani Sh bilioni 780 mwaka 2015 hadi Sh trilioni 1.8 katika mwaka wa fedha 2026/27.

Mfumo wa M-Mama, kwa upande mwingine, umewezesha zaidi ya rufaa 150,000 za dharura kwa akina mama na watoto wachanga hadi Agosti 2026.

Ndejembi amesema hatua hizo zinaonyesha umuhimu wa kuunganisha utashi wa kisiasa, rasilimali na utekelezaji katika kuboresha maisha ya wananchi.

Ajenda ya “SHE RISES”

Katika ngazi ya Bara la Afrika, Ndejembi amesema Rais Samia anaendelea kutumia nafasi yake kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto kusukuma utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika kuhusu afya ya mama, mtoto mchanga, watoto na vijana balehe.

Ajenda hiyo pia inahusisha dhana ya “sifuri tatu”, inayolenga kuondoa kujifungulia nyumbani, kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika pamoja na kuhakikisha watoto wanapata chanjo.

Kupitia SHE RISES, Tanzania pia inasisitiza umuhimu wa wanawake kutokuwa wapokeaji wa huduma za afya pekee, bali kushiriki katika uongozi na maamuzi yanayounda mifumo ya afya.

UNFPA na WHO Zapongeza Juhudi

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), Diene Keita, amepongeza uongozi wa Rais Samia na nafasi ya Tanzania katika kuiweka afya ya mama na mtoto kwenye ajenda ya kisiasa ya Afrika.

Keita amesema mafanikio katika eneo hilo yanahitaji utashi wa kisiasa unaoonekana kupitia bajeti, uwekezaji katika huduma za afya ya uzazi na kuimarishwa kwa nafasi ya wakunga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Mohamed Janabi, amesema dhamira ya kisiasa inapounganishwa na uwekezaji, uwajibikaji na vitendo, maisha ya mama na mtoto yanaweza kuendelea kuokolewa.

Janabi amesisitiza pia umuhimu wa wanawake katika mifumo ya afya, akisema wanawake wanachangia sehemu kubwa ya utoaji wa huduma za afya barani Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, wanawake ni takribani asilimia 70 ya watendaji katika sekta ya afya barani Afrika, lakini bado wanawakilisha takribani asilimia 25 katika nafasi za kufanya maamuzi.

Amesema SHE RISES inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika kutunga sera, kupanga bajeti, kuweka vipaumbele na kushika nafasi za uongozi katika sekta ya afya.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Afrika na nje ya bara hilo, viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau wa afya duniani pamoja na watunga sera.

Kwa Tanzania, ujumbe wa SHE RISES unaunganisha afya ya mama na mtoto na masuala ya uongozi, rasilimali, uwajibikaji na ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi yanayohusu mifumo ya afya.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
25 Septemba 2026
New York, Marekani