
Mwanamume mwenye umri wa miaka 63 nchini Marekani, Darrell Long, amepatikana na hatia ya jaribio la kumuua kwa makusudi mke wake wa zamani, Dawn, baada ya kumpiga risasi mara tano katika nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na mtoto wao wa kiume.
Long, mkazi wa Pennsylvania, alipatikana na hatia Jumanne, Septemba 22, 2026, kwa makosa mbalimbali likiwemo jaribio la mauaji ya daraja la kwanza, uvamizi wa nyumba, shambulio la kusababisha majeraha makubwa, shambulio kwa kutumia silaha na unyanyasaji.
Tukio hilo lilitokea Machi 25, 2025, baada ya Long kuvamia nyumba ya Dawn wakati akiwa amelala kwenye sofa sebuleni. Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Kaunti ya Lebanon, Pier Hess Graf, Long alimpiga Dawn usoni kwa kutumia bunduki kabla ya kumpiga risasi mara kadhaa.
Dawn alijaribu kujitetea na katika purukushani hiyo alifanikiwa kumng’ang’ania Long na kumwangusha chini. Hata hivyo, Long aliendelea kutumia bunduki hiyo na kumpiga risasi nyingine, ikiwemo moja iliyompiga mkononi na kusababisha jeraha kubwa kwenye kidole chake cha shahada.
Bunduki hiyo ilikwama wakati wa mapambano, lakini baada ya Long kujaribu kuirekebisha, alifanikiwa kuendelea kumpiga Dawn risasi. Mwathiriwa, akiwa amejeruhiwa katika sehemu kadhaa za mwili, alijikokota hadi chumbani na kujifungia.
Dawn alifanikiwa kupiga simu ya dharura 911 kwa kutumia Apple Watch yake baada ya kuvunja sehemu ya kifaa hicho ili kuanzisha huduma ya dharura.
Long alikimbia kutoka eneo la tukio kabla ya polisi kumkamata. Mwendesha mashtaka amesema alifunga mlango kabla ya kuondoka, jambo ambalo lingeweza kuchelewesha msaada kwa Dawn.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka, shambulio hilo lilihusishwa na mzozo kuhusu msaada wa malezi ya mtoto. Dawn aliwasilisha madai ya msaada wa malezi baada ya kuanza mchakato wa talaka mwaka 2023.
Pia imeelezwa kuwa katika mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, Long alimtumia mtoto wao jumbe 23 zenye maneno makali kuhusu Dawn, akitaka mtoto huyo amfikishie ujumbe mama yake ambaye alikuwa amemzuia Long kuwasiliana naye moja kwa moja.
Mmoja wa jumbe hizo, uliotumwa siku 17 kabla ya shambulio, ulidaiwa kuwa na tishio kwamba endapo Dawn angebadilika mwenendo, mtoto wao angeishia kuwapoteza wazazi wote wawili.
Mwendesha mashtaka Hess Graf amesema Long bado anaendelea kumlaumu Dawn kwa shambulio hilo, huku akidai kuwa hakujutia alichokifanya.
