Masauni ataka ubunifu kukabili tabianchi – HabariLeo

ARUSHA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amezitaka nchi za Afrika kutumia changamoto za mabadiliko ya tabianchi kuibua ubunifu, utafiti na maendeleo badala ya kujiona waathirika pekee.

Masauni ametoa wito huo jijini Arusha wakati akifunga Kongamano la Vyuo Vikuu Vitano lililofanyika katika Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST).

Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zinaonekana katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, maji, afya, miundombinu, nishati na mifumo ya ikolojia, hivyo ni muhimu ustahimilivu dhidi ya athari hizo kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo, tafiti na sera.

“Afrika haipaswi kuangalia changamoto ya tabianchi kwa mtazamo wa kuwa waathirika pekee. Tunapaswa pia kuangalia fursa, ubunifu na uongozi,” amesema Masauni.

Amesema hatua hiyo itasaidia nchi za Afrika kutumia maarifa na tafiti zinazozalishwa na taasisi za elimu ya juu katika kutafuta suluhisho la changamoto za tabianchi na kuimarisha maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu hazipaswi kubaki katika machapisho ya kitaaluma, bali zinapaswa kuwafikia wadau na kutumika kutatua changamoto zinazozikabili jamii.

“Utafiti pekee hautoshi. Utafiti lazima uwasilishwe, ueleweke na utumike na wadau,” alisema Profesa Kipanyula.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, watafiti na wadau mbalimbali ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanageuzwa kuwa suluhisho la vitendo kwa changamoto za maendeleo na mabadiliko ya tabianchi.