Na Bibi Maendeleo Irene Samora, Matukio Daima Media
UDUMAVU ni hali inayotokea pale mtoto anapokuwa na kimo au urefu mfupi ikilinganishwa na umri wake kutokana na kuathirika kwa ukuaji na maendeleo ya mwili.
Akizungumza katika kipindi cha Bibi Maendeleo kinachorushwa na Matukio Daima Media, Bibi Maendeleo Irene Samora Kijinga amesema tatizo hilo husababishwa zaidi na ukosefu wa lishe bora wa muda mrefu, magonjwa au maambukizi ya mara kwa mara, pamoja na mazingira yasiyofaa kwa ukuaji wa mtoto.
Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa udumavu hutokana na mchanganyiko wa lishe duni, maambukizi ya mara kwa mara na ukosefu wa malezi yanayochochea ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Kwa mujibu wa Irene, udumavu huathiri ukuaji wa mwili na uwezo wa mtoto kujifunza. Mtoto mwenye udumavu anaweza kuwa mfupi sana kulingana na umri wake, kuchelewa kuzungumza, kutembea au kuketi, kuchoka mara kwa mara na kukosa nguvu mwilini.
Amesema athari nyingine ni kupungua kwa uwezo wa mtoto kuelewa masomo na kufanya shughuli mbalimbali ,Hali hiyo inaweza kusababisha mtoto kuwa na maendeleo duni shuleni na kushindwa kufikia kikamilifu uwezo wake wa kimwili na kiakili.
Irene amesema chanzo kikuu cha udumavu ni ukosefu wa chakula chenye virutubisho vya kutosha, vikiwemo protini, vitamini na madini muhimu kama chuma. Magonjwa ya mara kwa mara na mazingira duni pia yanaweza kuathiri ulaji, ufyonzwaji na matumizi ya virutubisho mwilini.
Ameongeza kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kumweka mtoto katika hatari ya kupata udumavu ni kuzaliwa na uzito mdogo, kutonyonyeshwa vizuri maziwa ya mama na kupewa chakula cha nyongeza kisichokidhi mahitaji ya mwili wake.
Sababu nyingine ni mtoto kuugua mara kwa mara magonjwa kama kuhara, malaria na minyoo. Kutopata huduma muhimu za afya, zikiwemo chanjo na matibabu kwa wakati, kunaweza kuongeza uwezekano wa mtoto kuugua mara kwa mara na kuathiri ukuaji wake.
Irene amesema udumavu unaweza kuzuiwa kwa kumpatia mtoto lishe bora yenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali, vikiwemo nyama, samaki, mayai, maziwa, mikunde, mboga, matunda na nafaka kamili.
Aidha, wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata chanjo zote kwa wakati, wanapelekwa kupata matibabu ya haraka wanapougua na ukuaji wao unafuatiliwa mara kwa mara katika vituo vya afya.
Amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya afya na lishe kwa wazazi, walezi na jamii nzima ili kuzuia udumavu na kuhakikisha watoto wanakua vizuri kimwili na kiakili.
“Udumavu kwa watoto unatokana zaidi na ukosefu wa lishe bora na magonjwa ya mara kwa mara. Hivyo, kinga yake inaanzia katika lishe bora, malezi yanayofaa na upatikanaji wa huduma bora za afya,” amesema Irene.


