SHINYANGA: WAKULIMA mkoani Shinyanga wamepatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbegu na pembejeo za kilimo kuelekea msimu wa kilimo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Mali Shambani kupitia Programu ya Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi (AFDP).

Mafunzo hayo yametolewa Septemba 23, 2026, wakati wa Maonesho ya Pembejeo Bora na Mbegu Bora za Mazao (Innovation Seed Fair), yaliyoshirikisha wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Kuthibiti Mbegu Bora Tanzania (TOSCI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).

Maonesho hayo pia yameshirikisha wawakilishi wa kampuni mbalimbali zinazozalisha mbegu pamoja na wauzaji wa pembejeo za kilimo, kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata elimu na taarifa sahihi kuhusu pembejeo na mbegu wanazoweza kutumia katika uzalishaji.
Akizungumzia zoezi hilo, mtaalamu kutoka Wizara ya Kilimo, Ernest Kibulei, amesema mafunzo hayo yanatolewa Shinyanga Vijijini na Manispaa ya Kahama, kabla ya kuendelea mkoani Tabora katika Wilaya za Igunga na Nzega.

Amesema wataalamu hao wanatoa elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora, huduma ya upimaji wa afya ya udongo na kanuni bora za kilimo, pamoja na namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kibulei amesema elimu hiyo pia inahusisha maandalizi ya wakulima kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za El Niño, ili kuwawezesha kufanya maandalizi sahihi kabla na wakati wa msimu wa kilimo.
