TARURA YAOKOA BILIONI 124 UJENZI MADARAJA YA MAWE NCHINI

Dar es Salaam 

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 124 kutokana na ujenzi wa madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe.

Kiasi hicho cha fedha kimeokolewa kutokana na ujenzi wa madaraja ya mawe 527 kwa gharama ya shilingi bilioni 47 ambapo kama yangejengwa kwa kutumia nondo na zege yangegharimu zaidi ya shilingi bilioni 171.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Madaraja ya Mawe TARURA Makao Makuu, Mhandisi Mshauri Pharles Ngeleja wakati akitoa maelezo kwa mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega alipotembelea banda la TARURA katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wahandisi unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Sambamba na madaraja ya mawe, Mhandisi Ngeleja amemueleza Mgeni rasmi kuwa TARURA inajenga madaraja ya watembea kwa miguu “Suspension and suspended Bridge” kwenye barabara zilizosajiliwa na maeneo ambayo hayana mtandao rasmi wa barabara.

“TARURA tumeamua kujenga vivuko vya aina hii kwa ajili ya watembea kwa miguu lakini pia vina uwezo wa kutumika na waendesha baiskeli na bodaboda ambapo mpaka sasa vipo 80 na kwa kiasi kikubwa vimewasaidia wakulima kuyafikia masoko na huduma nyingine za kijamii kwa urahisi”, amesema Mhandisi Ngeleja.

Mhandisi Ngeleja ameongeza kuwa kwa sasa TARURA inatekeleza ujenzi wa vivuko hivyo mkoani Morogoro katika wilaya za Mvomero, Ulanga, Malinyi pamoja na wilaya ya Morogoro.

TARURA ambayo ni mdau mkubwa wa sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inashiriki katika Mkutano huo sambamba na kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya ujenzi kuhusu majukumu yake.