Global Publishers
September 24, 2026
894 views
0 Comments

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limechukua hatua dhidi ya mwandaaji wa shindano la Miss Grand Tanzania kwa tuhuma za kuendesha shindano hilo bila kuwa na kibali cha tukio kinachotakiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa matukio ya sanaa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, mwandaaji huyo alipewa notisi ya kosa hilo tarehe 12 Agosti 2026 na kutakiwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya siku 21.
Hata hivyo, BASATA imeeleza kuwa mwandaaji huyo hakutekeleza matakwa ya notisi hiyo ndani ya muda uliowekwa.

Kwa kuzingatia Kanuni ya 45 ya Kanuni za Baraza, BASATA imeamua kumtoza mwandaaji huyo faini ya Shilingi milioni tatu (TSh 3,000,000), ambayo anatakiwa kuilipa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
Aidha, BASATA imeamuru mwandaaji huyo kutokujishughulisha na kazi za sanaa kuanzia tarehe ya uamuzi hadi pale atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.
Hatua hiyo imekuja katika mazingira ambayo waandaaji wa matukio ya sanaa wanatakiwa kuzingatia taratibu na kupata vibali vinavyohitajika kabla ya kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa masharti ya mamlaka husika.

