Makamu wa Rais Ndejembi Alivyowasili New York Kumwakilisha Rais Samia UNGA81

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewasili jijini New York, nchini Marekani, kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81).

Makamu wa Rais amewasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy, ambako amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa – New York, Togolani Mavura, pamoja na maafisa mbalimbali.

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unawakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi mbalimbali kutoka mataifa wanachama, ambapo pamoja na mambo mengine, hujadili masuala ya kiuchumi, kisiasa, mazingira na haki za binadamu.

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu “Kurudisha Imani, Kusimamia Mabadiliko: Umoja wa Mataifa unaohudumia Wote” (Restoring Trust, Managing Transformation: A United Nations That Delivers for All).

Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha juhudi za kujenga upya uaminifu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, sambamba na kusimamia mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani, ikiwemo kasi ya maendeleo ya akili unde (AI).

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais anatarajiwa kuhutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, pamoja na kushiriki katika vikao mbalimbali, ikiwemo Mjadala Mkuu (General Debate), mikutano ya pembezoni na mikutano ya pande mbili (Bilateral Meetings).