RC Ruvuma Azindua Basi Jipya La Shilingi Milioni 334

Global Publishers
September 20, 2026
0 views
0 Comments

SONGEA, RUVUMA — Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amezindua basi jipya aina ya Coaster lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 334, lililonunuliwa kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Basi hilo limekabidhiwa rasmi kwa ofisi hiyo kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na kurahisisha shughuli za kikazi, hususan safari za watumishi katika ziara mbalimbali.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, RC Ahmed amewataka madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, pamoja na kuhakikisha gari hilo linafanyiwa matengenezo kwa wakati.

Amesema fedha zilizotumika kununua basi hilo ni za walipa kodi, hivyo watumishi wana wajibu wa kulilinda na kuhakikisha linatumika kwa manufaa ya umma.

RC Ahmed amesisitiza kuwa kuharibika kwa gari hilo mapema kutakuwa hasara kwa wananchi ambao wamechangia kupitia kodi zao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu, Joel Mbewa, amesema basi hilo litasaidia kupunguza changamoto za usafiri zilizokuwa zikiikabili ofisi hiyo.

Amesema basi hilo litatumika kusafirisha watumishi kwa pamoja wakati wa ziara mbalimbali, jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama za misafara.

Mbewa ameahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itahakikisha basi hilo linatunzwa ipasavyo, likifanyiwa service kwa wakati na kuendeshwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zote za usalama barabarani.