MASILE SACCOS YAWATAKA WANACHAMA KUREJESHA MIKOPO KWA WAKATI, YATANGAZA UCHAGUZI DESEMBA

Na Samwel Mpogole – Mbeya

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Masile SACCOS kilichopo Jijini Mbeya kimefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka, ambapo wanachama wamejadili mwenendo wa chama, changamoto zinazokikabili pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kukiendeleza.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkaguzi Mshauri wa Vyama vya Ushirika Kanda ya Mbeya, CPA Edson Pascal, amewataka wanachama wa Masile SACCOS kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati na kwa usahihi.

CPA Pascal amesema urejeshaji wa mikopo kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na uwezo wa kutoa huduma za mikopo kwa wanachama wengine, pamoja na kuimarisha uendeshaji wa SACCOS.

Kwa upande wake, Meneja wa Masile SACCOS, Rodina Mbwaga, amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa chama, ni muhimu kwa wanachama na viongozi kushirikiana katika kuzitafutia ufumbuzi.

Mbwaga amewataka wanachama kutoa ushirikiano kwa uongozi na kutoa maoni pamoja na ushauri pale inapohitajika, akisisitiza kuwa milango ya chama ipo wazi kwa wanachama.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Masile SACCOS, Venance Mlozi, amewataka wanachama kujiandaa kushiriki katika uchaguzi wa chama unaotarajiwa kufanyika Desemba 29, 2026.

Mlozi amesema ushiriki wa wanachama katika uchaguzi huo ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao katika uendeshaji wa chama, huku akiwataka kusoma na kuelewa kanuni pamoja na taratibu zinazohusu uchaguzi.

Baadhi ya wanachama walioshiriki mkutano huo wameeleza kufurahishwa na mwenendo wa Masile SACCOS, wakisema huduma zinazotolewa na chama hicho zimeendelea kuwapa fursa za kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Wanachama hao wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za chama, wakisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kuhakikisha Masile SACCOS inaendelea kukua na kuwanufaisha wanachama wake.