Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 03 Septemba, 2026, amezindua rasmi Jengo la Ramani la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililopo katika Mji wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo ambalo ni sehemu ya miundombinu ya kimkakati ya Jeshi, Dkt. Nyansaho amelipongeza JWTZ kwa kukamilisha mradi huo na kupata jengo la kisasa lililowekewa vifaa na teknolojia za kisasa zitakazowezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi na weledi zaidi.
Waziri Nyansaho amesema kukamilika kwa mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda uhuru, mamlaka na usalama wa nchi.
“Kukamilika kwa mradi huu wa kimkakati ni alama ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kutimiza majukumu yake ya ulinzi na usalama kwa ufanisi,” alisema Dkt. Nyansaho.
Aidha, Waziri Nyansaho amesema ana imani kuwa jengo hilo pamoja na vifaa vilivyowekwa vitatunzwa na kutumika ipasavyo, akieleza kuwa JWTZ limejijengea sifa kubwa katika utunzaji na usimamizi wa mali zake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, amemshukuru Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kulitambua na kulithamini Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kuliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Jenerali Mkunda pia ameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ushirikiano na usimamizi uliowezesha kufanikishwa kwa ujenzi wa jengo hilo, pamoja na kuwezesha wataalamu wa JWTZ kupata mafunzo maalumu kuhusu uendeshaji na matumizi ya mitambo ya kisasa iliyofungwa katika jengo hilo.
Awali, akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuzungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, amesema jengo hilo limejengwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na limewekewa mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kutengeneza ramani za kidijitali za 3D, pamoja na ramani za viwango vya juu zaidi kulingana na mahitaji ya kitaalamu.
Dkt. Mnyepe amesema uwepo wa jengo hilo na teknolojia hiyo ya kisasa utaongeza uwezo wa JWTZ katika utengenezaji, uchakataji na matumizi ya taarifa za ramani, hivyo kuchangia katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake ya kitaalamu na kimkakati.
Uzinduzi wa jengo hilo unaweka msingi muhimu katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia wa JWTZ, sambamba na juhudi za Serikali za kuendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kazi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usalama wa Taifa.
Mwisho









