Madiwani Tarime watakiwa kutanguliza maslahi ya wananchi
MARA: MKUU wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewataka madiwani na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuhakikisha wanakuwa viongozi bora kwa kutanguliza maslahi ya wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitia taarifa ya kufunga hesabu za halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika Agosti 26, 2026, Meja Gowele, alisema viongozi wanapaswa kutumia nafasi zao kuleta maendeleo badala ya kuwa sehemu ya matatizo katika jamii.
Alisema mafanikio ya halmashauri yanategemea ushirikiano kati ya viongozi, watumishi na wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa kuheshimiana na kusikilizana.

Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakisikiliza taarifa ya kufunga hesabu za halmashauri kwa mwaka 2025/2026
“Tuwe na utamaduni wa kuheshimiana na kusikilizana. Kiongozi asikilize wananchi wake na wananchi wasikilize viongozi wao. Hii ndiyo njia ya kujenga maendeleo endelevu,” alisema Meja Gowele.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo imeendelea kuimarika, lakini akawataka maafisa husika pamoja na madiwani kuendelea kushirikiana kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa.
“Suala la ulinzi na usalama limeimarika, hivyo natamani hali hii iendelee kwa kuelimisha wananchi, kuzungumza nao na kuzuia mambo yanayoweza kuvuruga amani katika maeneo yetu,” alisema.

Vyombo vya ulinzi na uslama
Aidha, aliwataka madiwani kusimamia kwa karibu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhujumu matumizi sahihi ya fedha za umma.
“Tunapokwenda katika miradi na kukukuta madiwani mmetia mkono katika ubadhirifu, tutachukua hatua bila kuangalia nafasi ya mtu. Jiepusheni na vitendo hivyo,” alionya.
Meja Gowele pia alihimiza halmashauri kuendelea kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato ili kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho, Matera Newland Chacha, aliwapongeza madiwani kwa kazi wanayoifanya na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya.
“Tutahakikisha tunaibua vyanzo vipya vya mapato, tunasikiliza kero za wananchi na kushiriki kikamilifu katika kutatua migogoro ili kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi wao,” alisema Chacha.
Pia alisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa fedha za umma katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuhakikisha mapato yatakayokusanywa yanatumika kwa miradi iliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi wa Tarime.