AFCON 2027,TANZANIA KUTANGAZA UTAMADUNI WAKE KUPITIA
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka Watanzania kutumia fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 kutangaza tamaduni za makabila mbalimbali nchini.
Malima alisema hayo wakati akifungua Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika mjini Morogoro, ambapo jumla ya washiriki 150,000 kutoka mikoa mbalimbali wanaonyesha na kutangaza tamaduni zao.
Alisema katika mashindano ya AFCON, miongoni mwa maeneo yanayotakiwa kutangazwa ni vivutio adimu vya utalii, sambamba na kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Malima alisema mashindano hayo yatahusisha Tanzania, Kenya na Uganda, huku Tanzania ikiwa mwenyeji wa baadhi ya michezo itakayofanyika Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuheshimu na kuthamini utamaduni wao, akisisitiza kuwa utamaduni ni sehemu muhimu ya heshima na utambulisho wa taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema Tamasha la Kitaifa la Utamaduni lilianza mkoani Dar es Salaam, kisha kufanyika Songwe na Ruvuma, kabla ya mwaka huu kufanyika Morogoro.
Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Msigwa aliwataka Watanzania kupuuza taarifa zisizo za kweli zinazoenezwa na baadhi ya watu kuhusu Tanzania kuondolewa kwenye uenyeji wa mashindano hayo.
Alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Baada ya ufunguzi wa tamasha hilo, kulifanyika Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Maadili uliolenga kuhamasisha na kuchochea maadili mema kwa Watanzania.
Mdahalo huo ulifanyika katika eneo la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambapo watoa mada walisisitiza umuhimu wa Watanzania kuwa kioo bora cha jamii kwa kuonyesha mfano mwema.
Wamesema maadili ni msingi wa utu, umoja na mshikamano wa kitaifa, hivyo Watanzania wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto na jamii kwa ujumla, kuipenda Tanzania kwa vitendo, kuheshimu utu na kujenga taifa lenye amani na mshikamano.
Maadili mema yameelezwa kuwa ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Watanzania.
Mwisho.

.jpeg)

.jpeg)

