WAZIRI MKUU AWASILI TANGA, MGENI RASMI KILELE CHA WIKI YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewasili leo Jumatatu, Agosti 24, 2026, katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Tanga, ambapo anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.

Amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Batilda Burian, pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda.

Alipowasili katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Waziri Mkuu ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea bunifu, teknolojia na kazi mbalimbali zinazowasilishwa na washiriki katika maadhimisho hayo.

 

Miss Universe kuhamasisha matumizi nishati safi – HabariLeo

DAR ES SALAAM; Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amewapongeza washiriki wa shindano la urembo la Miss Universe Tanzania kwa jitihada zao za kuwa mabalozi wa nishati safi ya Kupikia kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nishati hiyo nchini.

Naibu Waziri Salome amesema serikali itaendelea kushirikiana na jukwaa hilo muhimu katika kuifikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, huku akiwataka washiriki 33 wa shindano hilo kuwa chachu ya kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii, hususan katika maeneo ya vijijini.

Ametoa kauli hiyo Agosti 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa shindano la Miss Universe Tanzania kwa lengo la kupata warembo 20 watakaoendelea na hatua inayofuata ya mashindano hayo, kuelekea kumpata mwakilishi wa Tanzania katika shindano la Miss Universe duniani.

Amesema ushiriki wa warembo hao katika Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia unatoa fursa muhimu ya kuifikisha ajenda hiyo kwa makundi mbalimbali ya jamii na kuongeza uelewa kuhusu faida za kutumia nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.

Ameeleza kuwa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, inayopewa msukumo na Rais wa Tanzania, Dk  Samia Suluhu Hassan, inalenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka takribani asilimia 6 miaka michache iliyopita hadi asilimia 28.6 kwa sasa.

Amempongeza Mkurugenzi wa Taifa wa Miss Universe Tanzania, Millen Magese, kwa kuunganisha mashindano hayo na Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na kuwashukuru wadhamini wanaounga mkono jitihada hizo.

Pia ametoa wito kwa kampuni na wadau wengine kujitokeza kuunga mkono mashindano hayo ili yaweze kuwafikia wanawake wengi zaidi na kupanua wigo wa uhamasishaji.

Kwa upande wake, Magese amesema Miss Universe Tanzania imeamua kubeba ujumbe wa Nishati Safi ya Kupikia mwaka 2026 ikiwa ni sehemu ya ushirikiano na serikali katika kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Amesisitiza kuwa Miss Universe Tanzania itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha ujumbe wa Nishati Safi ya Kupikia unaendelea kuwa sehemu ya mashindano hayo kila mwaka, hivyo kuwapa washiriki nafasi ya kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.

Katika shindano hilo, washiriki walipata nafasi ya kutoa ujumbe mbalimbali kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, wakieleza umuhimu wa Watanzania kuhamia katika matumizi ya nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.

 

WANAFUNZI 95 WAENDA INDIA KUSOMEA AI, UHANDISI

 

Na Mwandishi Wetu

Zaidi ya wanafunzi 95 wa Kitanzania wameondoka nchini kuelekea India kuanza masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali, ikiwa ni kundi la kwanza kati ya wanafunzi 198 wanaotarajiwa kwenda kusoma nchini humo kupitia Global Education Link katika mwaka 2026.

Wanafunzi hao walioondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Terminal 3, jijini Dar es Salaam, wengi wao wamechagua programu zinazohusiana na sayansi, teknolojia na taaluma zinazohitajika katika dunia ya sasa, zikiwemo Computer Engineering, Cyber Security, Artificial Intelligence, Civil Engineering, programu mbalimbali za afya, sheria na biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Meneja wa Tawi la Dar es Salaam, Micky Musa, amesema kuondoka kwa wanafunzi hao ni sehemu ya mpango mpana wa kuwaunganisha vijana wa Tanzania na fursa za elimu ya kimataifa.

“Zaidi ya wanafunzi 95 wanaondoka katika kundi hili la kwanza kuelekea India, lakini kwa mwaka huu tunatarajia wanafunzi 198 kwenda kusoma nchini India. Hili si kundi la mwisho kwa sababu bado tuna wanafunzi wengine wanaoendelea kukamilisha taratibu zao,” amesema Musa.

Amesema mbali na India, Global Education Link inaendelea kuwaandaa wanafunzi wengine wapatao 185 wanaotarajiwa kuelekea nchini China, huku wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kwenda kusoma Malaysia, Marekani na Uingereza.

“Kadiri muda unavyokwenda Watanzania wataendelea kuona makundi mengine ya wanafunzi yakiondoka. Tunawaomba vijana wenye ndoto ya kusoma nje ya nchi wafike katika ofisi zetu zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Arusha. Muda bado upo. Njoo na matokeo yako, nasi Global Education Link tupo tayari kukusaidia kuifanya ndoto yako kuwa uhalisia,” amesema.

Musa pia amewataka wazazi na walezi wenye vijana wanaotamani kupata elimu nje ya nchi kutumia ofisi za Global Education Link kupata ushauri kuhusu uchaguzi wa vyuo, programu za masomo, udahili, visa na maandalizi ya safari.

Miongoni mwa wanafunzi walioondoka ni vijana wanaokwenda kusomea Computer Science Engineering, Artificial Intelligence na Cyber Security, wakisema wamechagua taaluma hizo kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Alvin Andrew Munda, mwenye umri wa miaka 17, anayeelekea Lovely Professional University nchini India, amesema amechagua Computer Science kwa sababu anataka kujenga ujuzi wa vitendo katika teknolojia na baadaye kujikita zaidi katika Cyber Security.

Amesema mfumo wa masomo wenye nafasi kubwa ya mafunzo ya vitendo na matumizi ya maabara ulimvutia kuchagua chuo hicho.

“Napenda mfumo wenye practical zaidi kuliko kusoma theory na kuandika mitihani pekee. Nataka nitumie elimu nitakayoipata kutengeneza suluhisho na baadaye nijikite katika Cyber Security kwa sababu usalama wa mtandao ni muhimu sana katika dunia ya sasa,” amesema.

Akimshukuru Global Education Link, Munda amesema taasisi hiyo imeisaidia familia yake katika mchakato mzima, kuanzia kupata chuo hadi kukamilisha maandalizi ya safari.

“Global imenisaidia katika process nzima kabisa. Wametuelekeza hatua moja hadi nyingine na wamekuwa kiungo kati yetu, wazazi wetu na chuo mpaka tumefikia hapa airport tayari kuondoka,” amesema.

Mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea masomo yanayohusiana na Computer Science na Artificial Intelligence amesema anatarajia kuwa mtaalamu wa data na teknolojia katika miaka ijayo.

Amesema AI imeanza kuwa sehemu muhimu katika benki, hospitali, biashara, serikali na sekta nyingine, na hivyo anaamini elimu katika eneo hilo itamwezesha kuwa sehemu ya maendeleo ya kiteknolojia nchini Tanzania.

Naye mwanafunzi anayekwenda kusomea programu jumuishi ya Bachelor of Business Administration na Bachelor of Laws amesema ana ndoto ya kuwa mwanasheria na mfanyabiashara mwenye mafanikio baada ya kumaliza masomo yake.

Amesema Global Education Link imechangia kwa kiasi kikubwa kumfikisha katika hatua ya kuondoka kwenda masomoni.

“Global Education imetusaidia sana, hasa kwenye visa processing, kupata chuo na maandalizi mengine ya safari. Ushirikiano kati yangu, wazazi wangu na Global ndio umetufikisha hapa leo,” amesema.

Wazazi waliowasindikiza watoto wao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pia wameipongeza Global Education Link kwa namna ilivyosimamia mchakato wa watoto wao kuanzia hatua za awali hadi siku ya safari.

Donald Kito, mzazi wa Isaac Donald Kito anayekwenda Lovely Professional University kusomea Diploma ya Civil Engineering, amesema familia yake ilifahamu huduma za Global Education Link kupitia matangazo na baada ya kuwasiliana nao walipata maelezo yaliyowapa imani ya kuendelea na mchakato.

Mwisho

Tundu Lissu Kuendelea Kujitetea Kesi ya Uhaini Leo Mahakamani

Shauri la uhaini namba 19605/2025 linalomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, linaendelea leo Agosti 24, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo inaendelea katika hatua ya ushahidi wa utetezi, mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Hatua hiyo ilianza Ijumaa, Agosti 21, baada ya Mahakama kumkuta Lissu ana kesi ya kujibu na kumpa nafasi ya kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Lissu, ambaye ameamua kujitetea mwenyewe, alianza kutoa ushahidi wake siku hiyo na pia akawasilisha orodha ya mashahidi anaotarajia kuwaita mahakamani.

Miongoni mwa mashahidi aliowataja ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais mstaafu, Philip Isdor Mpango; pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa.

Aidha, Lissu amewataja baadhi ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa CHADEMA, akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche, Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa na Brenda Rupia.

Leo, Lissu anatarajiwa kuendelea na ushahidi wake wa kujitetea kama shahidi wa kwanza. Baada ya kukamilisha ushahidi wake, mashahidi wengine wa upande wa utetezi wanatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wao.

Hata hivyo, suala la kuwaita viongozi wa Serikali, wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, limezua mvutano kati ya pande hizo mbili.

Upande wa mashtaka umepinga wito wa viongozi hao kufika mahakamani, ukieleza kuwa Jamhuri tayari imekamilisha ushahidi wake na kwamba si jambo la busara kumtaka Rais kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Kwa upande wake, Lissu amepinga hoja hiyo akisisitiza kuwa sheria inapaswa kutumika kwa kila mtu bila kujali cheo au nafasi yake.

Kesi hiyo inaendelea huku ikifuatiliwa kwa karibu kutokana na uzito wa mashtaka na majina ya viongozi wakuu wa Serikali yaliyotajwa kuwa sehemu ya mashahidi wa utetezi.

Iran Yatoa Onyo Kali Kuhusu Vikwazo Vipya vya Marekani

Iran imeonya kuwa nchi yoyote itakayounga mkono vikwazo vipya vya kiuchumi vinavyotarajiwa kutangazwa na Marekani dhidi ya Iran itachukuliwa kuwa imefanya kitendo cha vita.

Onyo hilo limetolewa na mkuu mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohsen Rezaei, wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka.

Rezaei amesema Iran iko tayari kulipiza kisasi kwa nguvu endapo Marekani itaendelea kuongeza shinikizo la kiuchumi. Pia ametishia kulenga njia nyingine za usafirishaji wa mafuta katika Ghuba ya Uajemi endapo hali itaendelea kuwa mbaya.

Wakati huo huo, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ameonyesha nia ya kuendelea na mazungumzo na Marekani. Amesema makubaliano ya awali yaliyofikiwa mwezi Juni ndiyo njia bora ya kuondokana na hali ya “si vita wala amani” iliyopo kati ya mataifa hayo.

Hata hivyo, kipindi cha siku 60 kilichowekwa kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kimekwisha bila kufikiwa kwa makubaliano mapya.

Mvutano pia umeendelea katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani. Hakuna mashambulizi yaliyothibitishwa katika eneo hilo katika saa 48 zilizopita, lakini idadi ya meli zinazopita imeendelea kuwa ndogo.

Iran pia imetangaza orodha ya meli kadhaa ambazo inasema zilikiuka masharti ya usafirishaji katika eneo hilo na inaweza kuziwekea faini au kuzizuia siku zijazo.

Katika juhudi za kupunguza mvutano, Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir, anatarajiwa kutembelea Tehran. Pakistan inajaribu kusaidia kuwarudisha Marekani na Iran kwenye meza ya mazungumzo.

Wakati hayo yakiendelea, hali ya Mashariki ya Kati bado ni tete. Mashambulizi yameripotiwa Gaza na Ukingo wa Magharibi, huku mtoto wa miaka minne akiuawa katika shambulio la anga la Israel huko Gaza, kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina.

Kwa ujumla, mvutano kati ya Iran na Marekani unaendelea kuwa tishio kwa usalama wa Mashariki ya Kati na pia kwa usafirishaji wa mafuta duniani, hasa kupitia Mlango wa Hormuz.

Mama Wa Miaka 18 Ashtakiwa kwa Mauaji Ya Mtoto Wake Wa Miaka Miwili

Mwanamke mwenye umri wa miaka 18, Devorah Diaz Perez.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 18, Devorah Diaz Perez, amekamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka miwili, katika jimbo la Georgia nchini Marekani.

Kukamatwa kwake kumekuja zaidi ya wiki mbili baada ya mpenzi wake wa kuishi naye, Celso Edison Vicente Y Vicente, mwenye umri wa miaka 22, kukamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya kukusudia pamoja na ukatili wa kiwango cha kwanza dhidi ya mtoto huyo.

Kwa mujibu wa Polisi wa Canton, tukio hilo lilianza kuchunguzwa Agosti 3, 2026, baada ya polisi kupokea taarifa ya mtoto mwenye umri wa miaka miwili kutokuwa na fahamu katika nyumba iliyopo eneo la Cartersville Street.

Celso Edison Vicente Y Vicente, mwenye umri wa miaka 22 mpenzi wake na Devorah Diaz Perez.

Mtoto huyo alipelekwa hospitalini kwa matibabu, lakini baadaye alitangazwa kuwa amefariki. Uchunguzi wa polisi uliendelea na kumhusisha Vicente Y Vicente, ambaye alidaiwa kuwa anahusika na kumtunza mtoto huyo siku ya tukio.

Hati za mashtaka zinadai kuwa Vicente Y Vicente alimpiga mtoto huyo kwa mikono na vitu vingine ambavyo havijafahamika, huku mtoto huyo akidaiwa kuwa na michubuko mingi mwilini, ikiwemo alama iliyofanana na chapa ya kiatu, pamoja na jeraha lililokuwa wazi kichwani.

Baada ya uchunguzi zaidi, polisi walimkamata pia mama wa mtoto huyo na kumshtaki kwa mauaji ya daraja la pili, makosa mawili ya ukatili dhidi ya watoto.

Polisi wamesema uchunguzi bado unaendelea na hawajatoa maelezo zaidi kuhusu ushahidi au mazingira ya kifo hicho kwa sababu kesi bado iko katika hatua za kisheria.

Ofisi ya Mchunguzi wa Kimatibabu ya Georgia Bureau of Investigation inatarajiwa kufanya uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo ili kubaini rasmi chanzo na namna ya kifo chake.

Polisi wa Canton wamesisitiza kuwa watu wote wanaoshtakiwa wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi pale watakapothibitishwa kuwa na hatia na mahakama.

Utata Wa Neema Na Mwajiri Wake Wafikia Mwisho, Zali Mapito Afika Oman Kufuatilia – Video

Global Publishers
August 24, 2026
984 views
0 Comments

Mtangazaji wa Global TV Online na 255 Global Radio, Zali Mapito, yupo nchini Oman kufuatilia hali ya binti mdogo wa Kitanzania, Neema Kengele, kutoka Geita, ambaye amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa siku kadhaa.

Akizungumza akiwa Oman katika mahojiano na mtangazaji God Muya wa Global TV, Zali ameeleza kwa kina hali inavyoendelea pamoja na juhudi zinazofanyika kuhakikisha Neema anapata msaada unaohitajika.

Katika maelezo yake, Zali amebainisha pia juhudi zinazofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Maulidah Hassan, katika kufuatilia na kusaidia katika suala hilo.

Ujio wa Zali nchini Oman unalenga kufuatilia kwa karibu maendeleo ya hali ya Neema pamoja na kupata taarifa sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa na mamlaka pamoja na wahusika mbalimbali katika kuhakikisha Mtanzania huyo anapata matibabu na msaada unaohitajika.

Hali ya Neema imeendelea kufuatiliwa kwa karibu, huku Watanzania wakisubiri taarifa zaidi kuhusu maendeleo yake.

Mfanyabiashara Afichua Siri ya Mafanikio ya Wakinga na Safari Yake ya Utajiri – Video

Global Publishers
August 24, 2026
1,608 views
0 Comments

Mfanyabiashara maarufu nchini, Hosiana Sanga, amefichua baadhi ya misingi anayoiamini kuwa imechangia mafanikio ya Wakinga katika biashara, huku akisimulia safari yake binafsi ya kutoka katika maisha magumu hadi kujenga utajiri.

Sanga ameeleza hayo katika mahojiano ya Hard Talk ya Global TV na mtangazaji Lillian Mwasha, ambapo amezungumzia kwa kina changamoto alizopitia, misingi ya mafanikio na uzoefu alioupata katika safari yake ya ujasiriamali.

Mfanyabiashara huyo amesema safari yake ya mafanikio haikuwa rahisi, akieleza kuwa alikua bila baba baada ya kumpoteza akiwa bado mdogo. Hata hivyo, changamoto hiyo haikumzuia kuendelea kupambana na kutafuta njia za kujenga maisha yake.

Katika mahojiano hayo, Sanga ameshirikisha uzoefu wake katika biashara na namna alivyoweza kuanza safari yake akiwa na uwezo mdogo, kabla ya kufikia hatua ya kujenga utajiri na kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wanaotambulika.

Ameeleza pia kuhusu utamaduni wa Wakinga katika biashara, akitaja misingi na mitazamo inayowasaidia watu kutoka jamii hiyo kujenga na kukuza biashara zao.

Kwa mujibu wa Sanga, mafanikio katika biashara yanahitaji zaidi ya mtaji, yakihusisha nidhamu, kujituma, uthubutu wa kuchukua hatua na uwezo wa kuvumilia changamoto zinazojitokeza katika safari ya ujasiriamali.

Simulizi yake imekuwa sehemu ya mazungumzo yanayolenga kutoa mtazamo wa ndani kuhusu maisha ya wafanyabiashara, changamoto wanazopitia na mambo yanayoweza kumsaidia mtu kujenga mafanikio yake hatua kwa hatua.

Dkt. Gwajima Aingilia Kati Sakata la Mobetto, Aonya Ukatili Mtandaoni

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa ujumbe wa kuunga mkono mapambano dhidi ya ukatili mtandaoni, huku akimpongeza msanii na mrembo Hamisa Mobetto kwa kuzungumzia changamoto hiyo hadharani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dkt. Gwajima amesema anatoa pole kwa watu wote waliofanyiwa au wanaoendelea kufanyiwa ukatili mtandaoni, akisisitiza umuhimu wa waathirika kutafuta msaada na kuchukua hatua stahiki.

Dkt. Gwajima pia amempongeza Hamisa Mobetto kwa kupaza sauti kuhusu suala hilo na kueleza kuwa yuko tayari kumsaidia kupata wataalamu watakaoweza kumsikiliza na kumpa ushauri.

Aidha, Waziri huyo ametoa onyo kwa watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya kumkatili Hamisa, akiwataka kutambua kuwa umaarufu na nafasi walizonazo havipaswi kutumiwa kuvuruga amani na ustawi wa wengine.

“Hivi mnaona raha sana kutumia fursa mlizonazo kuvunja amani za wengine? Hivi umaarufu wenu unafanyika kioo cha jamii au giza la jamii?” amehoji Dkt. Gwajima.

Amesema tabia za aina hiyo zinaweza pia kuibua masuala ya kisheria, akiwataka wanaokumbana na ukatili mtandaoni kutumia njia zinazotambulika kisheria, ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo husika na kupata msaada wa mawakili.

Dkt. Gwajima ameendelea kusisitiza umuhimu wa maadili katika matumizi ya mitandao ya kijamii, akisema maadili mabaya yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

Amehoji pia namna ambavyo baadhi ya wanajamii hushiriki au kushabikia maudhui yanayowajadili na kuwashambulia watu wengine, lakini wanapokumbwa na hali kama hiyo wao wenyewe hukimbilia kuomba msaada.

“Jamii bila maadili ni majanga na misiba. Tushirikiane kujenga maadili mema,” amesema.

Katika ujumbe wake, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa waathirika wa ukatili mtandaoni hawapaswi kukaa kimya, bali wanapaswa kutumia fursa zilizopo za kisheria na kupata msaada wa kitaalamu ili hatua zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka sheria.

Akiuhitimisha ujumbe wake kwa msisitizo, Waziri huyo ameuliza: “Niongeze sauti au imetosha?” huku akiahidi kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa maadili na matumizi salama ya mitandao ya kijamii.