Kiongozi wa upinzani Zambia kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani

Lusaka. Kiongozi wa upinzani Zambia, Brian Mundubile amesema atapinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa urais nchini humo, akidai kulikuwa na udanganyifu katika upigaji kura uliompa ushindi Rais Hakainde Hichilema kwa muhula wa pili wa uongozi.

“Kampeni yetu imebaini na kuweka kumbukumbu za kasoro kubwa, kutokuwiana kwa taarifa na mazingira yanayohusu namna uchaguzi ulivyoendeshwa, kura zilivyohesabiwa, matokeo yalivyowasilishwa na hatimaye kutangazwa,” amesema Mundubile katika taarifa yake aliyoitoa jana Jumatano Agosti 19, 2026 kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Reuters.

Ingawa uchaguzi huo uliofanyika Agosti 13, 2026 ulikuwa kwa kiasi kikubwa wa amani, upinzani unaeleza vitisho na vikwazo vilitawala kampeni zake, jambo lililoibua wasiwasi kutoka kwa waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) ilimtangaza Hichilema kuwa mshindi baada ya kupata takriban asilimia 60 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Agosti 13, huku Mundubile akipata asilimia 38.

Baada ya kipindi cha maandalizi ya uchaguzi kuwa tulivu kwa kiasi katika nchi hiyo yenye watu milioni 22, hali ya kisiasa ilianza kuwa na mvutano mkubwa mara baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa.

Mamlaka ziliwakamata watu 11, akiwemo baadhi ya viongozi wakuu wa upinzani, katika operesheni ya uvamizi iliyohusisha kurushiana risasi, wakati Mundubile akiwa eneo hilo.

Tume ya uchaguzi pia ilisimamisha kwa saa kadhaa shughuli ya kuhesabu kura kutokana na taarifa za vurugu dhidi ya maofisa wa vituo vya kupigia kura pamoja na wizi wa karatasi za kura.

Akizungumzia uchaguzi huo Jumatano, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Turk, alisema ana wasiwasi kuhusu kukamatwa kwa viongozi wa upinzani.

Turk alisema katika taarifa yake kwamba kukamatwa kwao lazima kuendane kikamilifu na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, pamoja na sheria za ndani za Zambia.”

Hichilema aliingia kwenye uchaguzi huo akiwa mgombea aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda, baada ya kuiongoza Zambia katika mabadiliko makubwa ya kiuchumi na mchakato wa kurekebisha deni la taifa.

Hata hivyo, muhula wake wa kwanza pia uliibua wasiwasi kuhusu nafasi ya kisiasa nchini Zambia, huku vyama vya upinzani na makundi ya kiraia vikiishutumu serikali yake kwa kubana sauti zinazokosoa utawala.

Muhula wa pili wa kiongozi huyo unatarajiwa kuathiriwa na shinikizo la kutaka uwajibikaji zaidi, umoja wa kitaifa na kuhakikisha manufaa ya ukuaji wa uchumi yanawafikia wananchi wengi zaidi.

Hichilema anatarajiwa kuapishwa ndani ya siku saba baada ya tume kuchapisha matokeo rasmi ya uchaguzi, ambayo yanapaswa kutangazwa ifikapo Agosti 24. Hata hivyo, hatua ya upinzani kupinga matokeo mahakamani inaweza kuchelewesha mchakato huo.