Mwili wa mwanamume wakutwa porini karibu na eneo la Jeshi Makuburi
Dar es Salaam. Mwili wa mwanamume umekutwa katika eneo la Makuburi, Dar es Salaam, ukiwa hauna jeraha lolote linaloonekana, huku jitihada za kuutambua zikishindikana hadi saa tano kamili leo.
Mwili huo umekutwa katika eneo linalodaiwa kuwa chini ya uangalizi wa jeshi, hali iliyosababisha Polisi, wanajeshi pamoja na wataalamu wa Red Cross kufika eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi na hatua za awali za utambuzi.
Mashuhuda wamesema taarifa za kuwepo kwa mtu huyo katika eneo hilo zilianza kusambaa tangu saa moja asubuhi, baada ya baadhi ya watu kumuona akiwa amelala.
Mmoja wa mashuhuda, James Pancras, amesema aliposogea eneo hilo alimkuta mwanaume huyo akiwa amelala, hajitambui.
“Nilisogea na kumkuta mwanamume huyo akiwa amelala,” amesema Pancras.
Shuhuda mwingine, Anamaria Jilala, amesema alitoa khanga yake kumfunika mwanaume huyo baada ya kuombwa msaada, akisema mwonekano wake haukuonesha dalili za jeraha.
“Nilipita hapa, nikaambiwa kuna mtu amefariki, nilitoa khanga yangu kumsitiri, lakini ukimuangalia ni mtu tu mwenye afya, hana jeraha lolote, ni kama amelala,” amesema Jilala.
Mwananchi imeshuhudia vikosi vya ulinzi na usalama katika eneo la tukio vikitaka watu kumtazama mwanamume huyo kwa lengo la kubaini iwapo kuna anayemfahamu, lakini hawakuruhusiwa kupiga picha.
Hata hivyo, hadi saa tano kamili asubuhu, hakuna mtu aliyemtambua kabla ya mwili huo kuondolewa.
Mjumbe wa Kata ya Makuburi, Kondo Juma Kondo, amesema hana taarifa kuhusu marehemu huyo, akieleza kuwa alifika eneo hilo baada ya kupigiwa simu na kupewa taarifa kuwa kuna mwili.
“Nimepigiwa simu kwamba kuna mwili hapa, ndiyo nimefika na kukuta hivi, sina ninachokijua zaidi kuhusu huyu mtu,” amesema Kondo.
Mwananchi ilishuhudia Kondo akifanya ukaguzi wa awali wa mwili huo, ikiwamo kuangalia iwapo ulikuwa na kitu chochote kinachoweza kusaidia katika utambuzi, lakini hakukuwa na kitu kilichobainika.
Mwanamume huyo alikuwa amevaa gambuti, suruali nyeusi na fulana nyekundu kuukuu, huku Polisi, wanajeshi na Red Cross waliendelea na hatua za ukaguzi wa eneo na mwili huo.
Hata hivyo, wakati wa kuondoa mwili huo, walimvua gambuti na miguu yake kukutwa ikiwa na matope, huku utambulisho wa marehemu pamoja na chanzo cha kifo ukisubiri hatua zaidi za mamlaka.

