Mama asimulia gharama za dialisisi zilivyokuwa mzigo kwa familia – 2
Singida/Dar. Nikiwa ndani ya Hospitali ya Makiungu, iliyopo Kijiji cha Makiungu, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, macho yangu yanavutiwa na mwanamke wa makamo aliyeketi kimya kwenye benchi la wagonjwa wa nje.
Mama huyo, aliyevalia kilemba cheusi na khanga nyeupe, anaonekana kuchoka. Macho yake yamejaa huzuni, huku mikono yake ikiwa imekunjwa kana kwamba anajaribu kujizuia kulia.
Namsogelea na kujitambulisha. Kwa sauti ya chini anasema, “Nimekuja kutibiwa shinikizo la juu la damu (presha).”
Hata hivyo, kadiri mazungumzo yanavyoendelea, ninagundua tatizo haliko kwenye presha pekee, bali ni maumivu ambayo hayapimwi kwa kifaa chochote cha hospitali.
“Presha hii imenianza baada ya kumzika mwanangu,” anasema Christina Hamis (69), mkazi wa Kijiji cha Muhintiri, Kata ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi, huku machozi yakianza kumtoka.
Miezi michache iliyopita alimzika mwanawe, Emmanuel Alute (35), aliyefariki dunia Mei 16, 2026, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kutokana na ugonjwa sugu wa figo baada ya kupambana kwa zaidi ya miaka miwili na matibabu ya dialisisi.
Anasema hayo yote yalitokana na kukosekana kwa huduma za kibingwa ndani ya Mkoa wa Singida.
Hata hivyo, Christina anaamini kama huduma hizo zingepatikana karibu na makazi yake, huenda simulizi ingekuwa tofauti.
“Kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ingekuwa na huduma hizi mapema, tusingekaa miaka miwili Dodoma tena ugenini kwa maji na chakula cha kununua, sahani ya chakula Sh9,000 kwa mlo mmoja wa mtu mmoja. Tusingeuza kila kitu. Huenda mwanangu angekuwa hai,” anaeleza.
Anasema kila safari ya mamia ya kilomita iliongeza gharama ambazo familia haikuweza kuzimudu. “Maskini anaumwa mara mbili. Mara ya kwanza ugonjwa, mara ya pili gharama.”
Christina, ambaye mwanawe alifariki dunia baada ya kukaa zaidi ya wiki moja katika chumba walichopanga bila kufanyiwa dialisisi baada ya kukosa Sh150,000, licha ya kulipia huduma hiyo kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo katika Hospitali ya BMH jijini Dodoma, anasimulia:
“Nilimfuata mhusika, akanijibu, ‘Mama, katafute hela.’ Nilimuomba sana kwamba nimelipia zaidi ya miaka miwili, nimeuza kila kitu na sasa nimeishiwa. Alisisitiza lazima nichangie gharama.”
Anasema ilimbidi amuache mgonjwa peke yake na kurudi Ikungi kutafuta fedha, na siku tano baadaye alipigiwa simu na majirani kuwa hali ya mwanaye imebadilika.
Christina anasema aliporudi Dodoma, licha ya kuwa na fedha mkononi, alimkuta mwanawe anakoroma na kabla hajaita bajaji kumuwahisha kwenye mashine ya dialisisi, alifariki dunia.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo za kuambiwa atafute hela, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, anasema, “Sijawahi kuwa na hii taarifa kama sababu ya kifo. Ni kushindwa kulipia dialisisi, maana tuna mwongozo wa Wizara ya Afya ambao huwa tunautumia kutoa idhini ya kupata matibabu kwa waliothibitika hawajiwezi.”
Akitoa ufafanuzi zaidi Agosti 13, 2026, Profesa Makubi anasema mfumo wa msamaha wa gharama za matibabu upo kisera na unatekelezwa kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya.
Anasema mwananchi anayeshindwa kumudu gharama hupewa fursa ya kufanyiwa tathmini ili kuthibitisha hali yake ya kiuchumi na kubaini kama anaangukia katika makundi yanayostahili msamaha.
Baada ya kuthibitishwa, mwananchi hupewa cheti cha msamaha na kuendelea kupata huduma kama kawaida hadi atakapotoka hospitalini. Mchakato huo unaweza kuchukua siku moja hadi tatu, kutegemea na tathmini.
Profesa Makubi anasema BMH husamehe gharama zinazofikia takriban Sh400 milioni kwa mwezi, zikiwamo dawa, vipimo na huduma za upasuaji.
Ugonjwa wa figo ulianza kwa ajali
Baada ya mazungumzo yangu na Christina, nilishawishika kufahamu zaidi, hivyo tukaongozana kutoka Makiungu mpaka katika kijiji anachoishi kwa lengo la kukutana na familia yake.
Baada ya safari ya takribani kilomita 40 kwa mwendo wa pikipiki kutoka Hospitali ya Makiungu hadi Kijiji cha Muhintiri, tunaketi na ananieleza kwa kina, akisema kifo cha Emmanuel hakikuua mtoto wake pekee, bali kilizika pia uchumi wa familia nzima.
“Nimeuza kila kitu. Mashamba, ng’ombe, kibanda, hata nyumba niliyokuwa najenga ilisimama kama unavyoona. Leo hii nimebaki sina kitu,” anasema.
Kisa cha Emmanuel hakikuanza na figo. Mwaka 2014, akiwa mchimbaji mdogo wa dhahabu huko Ikungi, alifukiwa na mawe mgodini na kuvunjika mgongo karibu na eneo la figo.
Baba yake, Yohana Alute, anasimulia kwamba walimkimbiza Hospitali ya Puma kabla ya kuhamishiwa Mtimaru na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro (KCMC), Moshi, ambako alitibiwa kwa karibu mwaka mzima.
“Baada ya kurudi nyumbani alikuwa anatembea kwa magongo, baadaye kwa bakora. Polepole alianza kujitegemea tena,” anasimulia.
Familia iliingia gharama kubwa hata kabla ya ugonjwa wa figo kuanza. “Niliuza ng’ombe wengi ili kumtibu. Nilidhani tumeshamaliza matatizo.”
Lakini mwisho wa mwaka 2023, Emmanuel alianza kulalamika maumivu makali ya kifua na kushindwa kupumua. Alipelekwa Hospitali ya Makiungu. Familia ilipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
“Tuliondoka Makiungu kwa ambulensi akiwa anahema kwa shida. Hata daktari alisema hakuwa na uhakika kama angefika akiwa hai,” anasimulia baba yake. Kwa bahati nzuri walifika, lakini hapo ndipo safari ya mateso ilipoanza.
Miaka miwili ya kuishi hospitalini
Christina anasema tangu Machi 2023 maisha yake yalihamia Dodoma.
Kwa siku 10 za mwanzo, Emmanuel alikuwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), huku gharama zikiongezeka kila siku; na baada ya kutoka ICU, alianza dialisisi mara tatu kwa wiki.
“Nikapanga chumba Ujasi Ng’ona. Kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa nilikuwa nampeleka dialisisi.
“Kila wiki tulilipia Sh750,000 kabla ya gharama kushuka. Gharama nyingine hazikuisha; bajaji ya kwenda na kurudi hospitalini ilikuwa Sh4,000 kwa siku. Mbali na chakula na maji, kulikuwa na kodi ya nyumba, vipimo, dawa, damu na gharama nyingine zisizokoma. “Niliishi asubuhi nikifikiria dialisisi, jioni nikifikiria nitapata wapi fedha ya wiki inayofuata,” anaelez amama huyo.
Christina anasema hata baada ya kukata bima ya afya aliyoshauriwa na madaktari, bado alibaki analipa kiasi kikubwa cha fedha. “Niliendelea kuuza mali moja baada ya nyingine. Mwisho nikabaki sina chochote,” anaeleza.
Anasimulia kuwa katika miezi ya mwanzo ndugu na watoto wengine walichangia fedha, lakini siku zilivyosonga, uwezo wao ukaisha.
“Mwanzoni walikuwa wanapiga simu kila siku. Baadaye simu zikaanza kuzimwa. Watu walikuwa wamechoka,” anasema, huku akisema hakuwalaumu. “Kila mtu ana maisha yake, lakini mzigo wote ukabaki mabegani kwangu. Nilibaki mimi na mwanangu.”
Mei 2026, bima ilimalizika muda wake, hospitali ilimtaka aanze tena kulipa gharama kubwa za dialisisi, Christina anasema aliomba msaada kwa viongozi wa hospitali.
“Niliwaambia sina tena kitu. Nimeuza kila nilichokuwa nacho.”
Anasema alipewa muda mfupi kutafuta fedha, akalazimika kurejea Singida kuuza chochote kilichokuwa kimebaki. Alipokuwa akihangaika kutafuta fedha, Emmanuel alimuacha peke yake katika chumba alichopanga. Anasema usiku wa Mei 15 alipigiwa simu kuwa hali yake imebadilika.
Asubuhi ya Mei 16 alirejea Dodoma. Alipomuona Emmanuel, alianza kumuita mama yake. “Mama, nakufa… niombee.” Christina anasema alipiga magoti pembeni mwa kitanda.
“Nikaanza kuomba. Nilipofumbua macho nikakuta anakoroma. Dakika chache baadaye alikuwa amefariki,” anasimulia, kwamba wanafunzi waliokuwa wamepanga nyumba hiyo walikuja baada ya kusikia kilio chake. Hata hivyo, alinyanyuka na kuanza kupambana kurudi na mwili wa mwanaye nyumbani (anaanza kulia kwa kwikwi).
Baba naye alibaki na majeraha. Alute naye hakuficha maumivu. Anasema zaidi ya ng’ombe 20 waliuzwa kugharamia matibabu ya mwanawe.
Nyumba aliyokuwa anajenga ilisimama, mifugo iliisha, uchumi ukaanguka. “Lakini bado hatukuweza kumuokoa.”
Anasema walipofikiria kumhamisha Emmanuel kutoka Dodoma kwenda Makiungu baada ya huduma za dialisisi kuanza kupatikana, gharama zilikuwa bado kubwa kiasi cha kushindwa kuanza upya mchakato wa matibabu. “Tuliona tubaki pale Dodoma hadi mwisho.”
Katika Kijiji cha Muhintiri, kwa waliomfahamu Emmanuel, alikuwa mchimbaji aliyewahi kuwapa nafasi vijana wengine kufanya kazi kwenye eneo lake la uchimbaji na hata alipopata jiwe lenye thamani ya Sh70 milioni alisaidia wengi.
“Alikuwa golikipa wa timu ya kijiji, kijana aliyependwa,” anasema mmoja wa vijana kijijini hapo.
Baada ya kifo chake, kijiji kilichanga fedha za mazishi, wakiwamo marafiki zake na wachimbaji wenzake pia. “Hakuwa na maadui, alikuwa mtu wa watu,” anasema mama yake.
Leo Christina anarudi Hospitali ya Makiungu kama mgonjwa. Anasema tangu alipompoteza mwanawe amepata shinikizo la damu, maumivu ya kichwa yasiyoisha na tatizo la kuona kwa jicho moja.
“Maumivu haya hayaishi. Kila nikikumbuka alivyoniambia, ‘Mama, nakufa, niombee,’ moyo unauma upya.”
Anatazama mbali, akisema mwanawe alikuwa anatoka kwenye mashine ya dialisisi akiwa amechoka baada ya saa tano za matibabu.
Christina anataka simulizi yake iwe fundisho. “Asipatikane mama mwingine atakayelazimika kuuza kila kitu, kukesha hospitalini miaka miwili, halafu mwisho arudi nyumbani na jeneza la mwanawe.”
Ananyamaza kwa sekunde chache, kisha anasema, “Mimi nilipoteza mtoto, lakini sitaki familia nyingine ipitie njia niliyopita.”

