DC Magoti awaahidi ajira vijana wa Mgambo Kisarawe
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani wani, Petro Magoti, ametoa matumaini kwa vijana wa wilaya hiyo wanaoshiriki mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba, maarufu Mgambo, kuwapa kipaumbele cha kwanza katika fursa mbalimbali za ajira pindi watakapohitimu kozi hiyo.
Magoti ametoa ahadi hiyo jana, Agosti 17, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya Mgambo katika Kijiji cha Kazimzumbwe.
Amewataka vijana hao kuzingatia mafunzo na nidhamu ya kijeshi, akisisitiza suala la ajira lipo chini yake.
Askari wanafunzi wa Jeshi la akiba wakiwa wamekaa wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Kisarawe katika ufunguzi wa mafunzo Augosti 17,206. Picha na Jumanne Bakana.
Pia, amewataka vijana hao kuwa na nidhamu, kudumisha uzalendo na kujituma kwa kufuata maelekezo ya wakufunzi.
“Wenzenu waliomaliza mafunzo mwaka jana walikuwa 152 na wote tuliwaajiri. Kisarawe ni moja ya wilaya ambayo askari wetu wa Jeshi la Akiba mnapitishwa kwenye uzalendo na mafunzo ambayo hayana mfano katika wilaya nyingine.
“Ndiyo maana, askari wetu wa Jeshi la Akiba wameendelea kuliliwa kila mahala. Tuliwaajiri hadi tukachukua wenzetu wa Jeshi la Akiba Mafia. Hata jana kuna kampuni imeomba vijana 18, kwa hiyo naomba niwahakikishie, kuweni na nidhamu, kuweni waadilifu, kuweni wazalendo, suala la ajira tuachieni,” amesema Magoti.
Askari wanafunzi wa Jeshi la akiba wakiwa wamekaa wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Kisarawe katika ufunguzi wa mafunzo Augosti 17,206. Picha na Jumanne Bakana.
Naye Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kisarawe, Stafu Sajenti Neema Ochieng, amesema mafunzo hayo yalianza Julai 8, 2026, kukiwa na vijana 85, kati yao wa kike wakiwa 22.
Ochieng amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki kujiamini na kujitoa kwa Taifa lao.
“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea washiriki ujuzi, maarifa, uzalendo na namna ya kudumisha ulinzi wa Taifa lao,” amesema Ochieng.
Kwa upande wake, Diwani wa Kazimzumbwe wilayani Kisarawe, Siza Dilunga, amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuendelea kuwatafutia vijana ajira kutoka katika kampuni mbalimbali.
“Ninakushukuru wewe mkuu wa wilaya kwa jitihada zako ambazo umekuwa ukiwapambania vijana, wananchi wa Kazimzumbwe na Kisarawe kwa ujumla. Umetoka kutuambia namna ambavyo unazungumza na kampuni kuja kutoa ajira kwa vijana wetu,” amesema Dilunga.

